SELF YALENGA KUINUA WANANCHI KUPITIA MIKOPO
Na Mwandishi Wetu-Dar es Salaam
Mfuko wa Taifa wa Huduma Ndogo za Kifedha (SELF Microfinance Fund) umeeleza kuwa unaendelea kutumia mikopo kuwa nyenzo ya kuwawezesha wananchi kuanzisha na kukuza shughuli za kiuchumi, kuongeza kipato na kujenga ajira nchini.
Akizungumza na wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa SELF, Santieli Yona, amesema katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2023 hadi 2026, mfuko huo umetoa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 138 kwa wanufaika 131,312, hatua iliyochochea shughuli za kiuchumi na kusaidia kutengeneza ajira 262,624.
Amesema SELF imekuwa ikiwafikia wajasiriamali wadogo, wakulima, wafugaji, wavuvi pamoja na makundi mengine, huku ikiwezesha SACCOS na AMCOS kupata fedha za kuwakopesha wanachama wao. Aidha, mfuko huo unatoa mikopo ya makazi na kwa watumishi wa umma, pamoja na mikopo inayowawezesha vijana kumiliki vyombo vya usafiri kama bajaji kwa ajili ya kujipatia kipato.
Yona amesema katika kipindi hicho SELF imepata faida ya Sh bilioni 3.19 na kutoa gawio la Sh milioni 490 kwa Serikali. Ameongeza kuwa huduma za mfuko zimeendelea kusogezwa karibu na wananchi kupitia matawi 12 na vituo viwili vya huduma vilivyofunguliwa mikoa ya Kigoma na Katavi, huku elimu ya fedha ikiendelea kutolewa kwa wanufaika ili kuwawezesha kutumia mikopo kwa malengo yaliyokusudiwa na kufanya marejesho kwa wakati.
Kwa upande wa mipango ya baadaye, Yona amesema SELF inalenga kupanua huduma za kidijitali ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa na huduma za mikopo bila wananchi kulazimika kufika katika matawi.
Amesema pia mfuko utaendelea kutoa elimu ya fedha, kuhamasisha urasimishaji wa biashara na kutoa mikopo ya majiko yanayotumia umeme, hatua zinazolenga kuongeza ufanisi wa biashara, ajira, matumizi ya nishati safi na kukuza uchumi jumuishi.
