PARACHICHI: ‘DHAHABU YA KIJANI’ INAYOWEZA KUBADILI MAISHA YA WAKULIMA
Na. Wellu Mtaki
KILIMO cha parachichi kinaweza kuwa chanzo cha uhakika cha kipato kwa wakulima kutokana na uwezo wa zao hilo kuendelea kuzaa kwa miaka mingi, huku uzalishaji ukiongezeka kadiri miti inavyokua na kukomaa.
Hayo yamesemwa na Moses Mlowe, Meneja wa Itecado, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Mkutano wa Tatu wa Kitaifa wa Wadau wa Tasnia ya Parachichi, ambapo amewahimiza wananchi kutokuona kilimo hicho kama uwekezaji unaohitaji kuanza na mashamba makubwa.
Mlowe amesema mkulima anaweza kuanza na idadi ndogo ya miti na kuongeza uzalishaji kadiri anavyopata uzoefu na uwezo wa kifedha.
Amesema parachichi limekuwa likitajwa kama “dhahabu ya kijani” kutokana na fursa zake za kiuchumi, lakini mafanikio katika kilimo hicho yanategemea maandalizi sahihi tangu hatua ya kuchagua eneo, kupima afya ya udongo, kupata miche bora hadi matunzo ya miti baada ya kupandwa.
“Parachichi kama mimea mingine linahitaji mwanga, maji na virutubisho. Kwa hiyo, ni muhimu mkulima kufahamu afya ya udongo kabla ya kuanza uzalishaji,” amesema Mlowe.
Mti huanza kuzaa baada ya miaka mitatu
Kwa mujibu wa Mlowe, mti wa parachichi unaweza kuanza kutoa mazao baada ya takribani miaka mitatu tangu kupandwa, huku uzalishaji ukiendelea kuongezeka kadiri mti unavyokua na kukomaa.
Amesema hali hiyo inalifanya zao hilo kuwa na uwezo wa kumpatia mkulima kipato cha muda mrefu iwapo atazingatia kanuni bora za kilimo na matunzo ya miti.
Mlowe amesisitiza umuhimu wa kutumia miche bora pamoja na teknolojia ya grafting (upandikizaji wa kikonyo), hasa kwa wakulima wanaolenga kupata aina maalumu ya parachichi yenye sifa wanazozihitaji.
Amesema kikonyo kinapaswa kuchukuliwa kutoka kwenye mti mama wenye afya na unaozaa vizuri, kwa kuwa hatua hiyo husaidia kuendeleza sifa bora za mti huo katika mche mpya.
Mlowe amewataka wananchi kutokuona kilimo cha parachichi kama uwekezaji unaohitaji kuwa na mashamba makubwa tangu mwanzo, akisema wanaweza kuanza na miti michache na kuongeza idadi kadiri wanavyopata uzoefu na rasilimali.
Amesema mkulima mwenye miti michache anaweza kuanza kupata kipato baada ya miti hiyo kuanza kuzaa, huku mapato yakiongezeka kadiri idadi ya miti na uzalishaji vinavyoongezeka.
Kwa upande wa kilimo cha kibiashara, amesema kampuni yao hupanga mashamba kwa kuzingatia nafasi maalumu kati ya mche na mche, pamoja na mstari na mstari, hatua inayosaidia miti kukua vizuri na kurahisisha shughuli mbalimbali za shamba.
Mlowe pia amesisitiza umuhimu wa kupunguza urefu wa miti ili kudhibiti ukuaji wake na kuzuia miti kuwa mirefu kupita kiasi.
Amesema hatua hiyo husaidia katika utunzaji wa miti na kurahisisha uvunaji wa matunda kwa sababu miti hubaki katika urefu unaoweza kufikiwa kwa urahisi.
Kwa mtazamo huo, amesema hata watoto wanaweza kusaidia katika shughuli za uvunaji bila kulazimika kupanda kwenye miti mirefu, jambo linaloweza kupunguza changamoto na hatari wakati wa mavuno.
Pamoja na fursa zilizopo, Mlowe amesema wakulima wa parachichi bado wanakabiliwa na changamoto za miundombinu, hususan barabara na umeme katika maeneo ya vijijini ambako mashamba mengi yanapatikana.
Amesema ukosefu wa barabara nzuri unaweza kuathiri usafirishaji wa parachichi kutoka mashambani kwenda sokoni, hasa kwa kuwa ni zao linalohitaji kusafirishwa kwa wakati ili kupunguza uwezekano wa kuharibika.
Kuhusu umeme, amesema upatikanaji wake vijijini umeendelea kuimarika, lakini baadhi ya mashamba yaliyo ndani zaidi bado yanahitaji nishati mbadala kama umeme wa jua (solar) kwa ajili ya kusukuma maji kutoka kwenye vyanzo vya maji kwenda mashambani.
Amesema kuboreshwa kwa barabara na upatikanaji wa nishati kutawasaidia wakulima kuongeza ufanisi wa uzalishaji, kurahisisha usafirishaji na kuongeza thamani ya biashara ya parachichi.
Sambamba na hilo, Mlowe amesema thamani ya parachichi haipo katika matumizi ya tunda hilo kama chakula pekee, bali linaweza kutumika pia katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali, ikiwemo mafuta yanayotumika katika shughuli tofauti.
Amesema kuongeza thamani ya parachichi ni eneo muhimu linaloweza kuongeza fursa za kiuchumi kwa wakulima na wadau wengine katika mnyororo wa thamani wa zao hilo.
Amesisitiza kuwa mkulima anayelenga kupata mavuno bora anapaswa kuzingatia haua zote muhimu, kuanzia uchaguzi wa eneo na miche, maandalizi ya mashimo, upandaji, upatikanaji wa maji na virutubisho hadi udhibiti wa magonjwa na wadudu.
“Ukitaka kuingia kwenye kilimo cha parachichi, anza kwa kuchagua miche bora, eneo linalofaa, zingatia afya ya udongo, maji na matunzo ya miti. Hapo ndipo unapoongeza nafasi ya kupata mavuno mazuri na manufaa ya kiuchumi,” amesema.
Kwa ujumla, Mlowe amesema kilimo cha parachichi kinaweza kuwa fursa muhimu ya kuongeza kipato kwa kaya na kuchochea shughuli za kiuchumi vijijini, iwapo wakulima watawekeza katika miche bora, teknolojia sahihi za uzalishaji na usimamizi mzuri wa mashamba.


