Breaking News

OFISI YA MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM YATOA UFAFANUZI KUHUSU VIDEO INAYOSAMBAA MITANDAONI


 


Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam inatoa ufafanuzi kuhusu video inayosambaa mitandaoni ikinukuu kauli ya Mkuu wa Mkoa, Mhe. Albert Chalamila, kuhusu madereva. Ofisi inafafanua kuwa video hiyo imesambazwa ikiwa imekatwa na kuishia katika sehemu ya kauli, hivyo kutoa tafsiri isiyokamilika ya ujumbe uliotolewa.

Katika video kamili, Mkuu wa Mkoa alitoa maelekezo na onyo kwa madereva kuhusu wajibu wa kufuata taratibu na maelekezo halali ya mamlaka, hususan katika maeneo ya stendi. Alisisitiza kuwa dereva ndiye anayewajibika wakati wa kuendesha gari na kwamba kutii maelekezo ya mwajiri au tajiri kinyume na taratibu hakuondoi wajibu wake wa kisheria.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa inawasihi wananchi na watumiaji wa mitandao ya kijamii kuzingatia video na taarifa kamili kabla ya kutoa tafsiri au hitimisho kuhusu kauli za viongozi, ili kuepuka upotoshaji unaoweza kusababishwa na kusambaza vipande vya video bila muktadha wake.