Breaking News

HESLB YAONGEZA FURSA ZA MIKOPO KWA WANAFUNZI

 



Na Mwandishi Wetu-Dar es Salaam

Wanafunzi wa elimu ya juu nchini wanaendelea kupata fursa kubwa zaidi za kugharamiwa masomo baada ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuongeza fedha zinazotengwa kwa ajili ya mikopo na ufadhili katika mwaka wa masomo 2026/2027.

Akizungumza Oktoba 12, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill M. Kiwia, amesema ongezeko la fedha za mikopo linatarajiwa kuwawezesha wanafunzi wengi zaidi kupata elimu ya juu bila kukabiliwa na changamoto kubwa za gharama za masomo.

Amesema katika awamu ya kwanza ya upangaji mikopo kwa mwaka huu, wanafunzi 165,775 wamepangiwa mikopo na ruzuku zenye thamani ya Sh535.7 bilioni, huku wanafunzi 74,769 wa mwaka wa kwanza wa shahada ya awali wakipangiwa mikopo ya Sh246.88 bilioni.

Kwa upande wa wanafunzi wanaoendelea na masomo, Dkt. Kiwia amesema wanafunzi 79,115 wa shahada ya awali wamepangiwa mikopo yenye thamani ya Sh252.4 bilioni, huku wanafunzi 8,538 wa stashahada wakipangiwa Sh22.9 bilioni. Aidha, wanafunzi 873 wamepangiwa ruzuku kupitia Samia Scholarship.

Amesema HESLB itaendelea kupanua wigo wa mikopo na ufadhili kwa kuzingatia mahitaji ya wanafunzi pamoja na vipaumbele vya taifa, huku akisisitiza umuhimu wa urejeshaji wa mikopo ili fedha hizo ziendelee kuwafikia wanafunzi wengine wenye uhitaji.