COPRA YATAKA VIUNGO VIONGEZE THAMANI, WAKULIMA WANUFAIKE ZAIDI
Na Wellu Mtaki
Wakulima na wafanyabiashara wa viungo nchini wametakiwa kutumia fursa za usindikaji, uongezaji thamani na masoko ili kuongeza kipato kutokana na mazao yao, badala ya kutegemea kuuza mazao ghafi yanayoweza kuuzwa kwa bei ya chini.
Wito huo umeibuka katika mdahalo ulioandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), uliowakutanisha wadau wa viungo kujadili mikakati ya kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao hayo, ikiwemo kuboresha masoko na kupanua fursa za biashara ndani na nje ya nchi.
Mdahalo huo umefanyika katika maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani mwaka 2026, yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Shule ya Msingi Usagara jijini Tanga.
Katika majadiliano hayo, wadau wamejadili umuhimu wa kuboresha uzalishaji na usindikaji wa viungo ili kuzalisha bidhaa zenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko la ndani na la kimataifa.
Hatua hiyo inalenga kuongeza ushindani wa bidhaa za viungo, kupanua wigo wa masoko na kuwawezesha wakulima pamoja na wafanyabiashara kunufaika zaidi na shughuli zao za kiuchumi.
Aidha, ushirikiano kati ya COPRA na wadau wa sekta ya viungo umeelezwa kuwa muhimu katika kujenga mnyororo wa thamani unaoweza kuongeza manufaa ya kiuchumi kwa wote wanaojihusisha na uzalishaji, usindikaji na biashara ya viungo.
Kupitia juhudi hizo, sekta ya viungo inatarajiwa kuwa na fursa zaidi za kukuza biashara na kuongeza thamani ya mazao, huku ikichangia kuboresha kipato cha wakulima na kuimarisha uchumi.




