DKT. MWIGULU ATETA NA MKURUGENZI MKUU WA FAO
Ataja umwagiliaji, zana za kisasa za kilimo na uongezaji thamani kuwa maeneo ya kimkakati
Na Mwandishi Wetu – Roma, Italia
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali imejipanga kuongeza uwekezaji katika umwagiliaji, uzalishaji wa mbegu kwa wingi na matumizi ya zana za kisasa za kilimo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha sekta ya kilimo nchini.
Dkt. Mwigulu ameyasema hayo leo, Jumatatu, Septemba 21, 2026, wakati akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Dkt. Qu Dongyu, kuhusu mageuzi ya mifumo ya chakula na kilimo nchini Tanzania.
Mazungumzo hayo yamefanyika jijini Roma, Italia, ambako Waziri Mkuu anashiriki Mkutano wa Kimataifa wa Kujadili Afya Moja na Mifumo ya Chakula na Kilimo unaofanyika katika Makao Makuu ya FAO.
Amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeongeza uwekezaji katika sekta ya kilimo na kuelekeza nguvu kwenye miradi ya kimkakati, ikilenga kuhakikisha wakulima wanapata zana bora za kilimo pamoja na huduma stahiki katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Dkt. Mwigulu amesema Tanzania ina fursa kubwa ya kuongeza uzalishaji kutokana na uwepo wa ardhi na vyanzo vya maji, hivyo Serikali inalenga kutumia rasilimali hizo kujenga mifumo ya kilimo inayostahimili mabadiliko ya tabianchi.
“Tanzania inalenga kuacha kuuza bidhaa ghafi, ambazo zimekuwa zikileta changamoto tunapokutana na misukosuko katika masoko ya dunia. Tunataka kuongeza thamani ya mazao na kuwa na masoko yenye ushindani,” amesema.
Aidha, amesema Tanzania inaendelea kutumia teknolojia za kidijitali katika kuwaandikisha wakulima na wasambazaji wa pembejeo, hatua inayolenga kuboresha upatikanaji na usambazaji wa zana za kilimo, mbolea na huduma nyingine kwa wakulima.
Akizungumzia mipango ya baadaye katika sekta hiyo, Dkt. Mwigulu amesema Tanzania inalenga kuelekeza nguvu kwenye programu chache za kimkakati zitakazotoa matokeo makubwa na yanayopimika, ikiwemo kuhamasisha uwekezaji na upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya mageuzi ya sekta ya kilimo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Dkt. Qu Dongyu, ameitaka Serikali ya Tanzania kuongeza uwekezaji kwa wanasayansi na watafiti chipukizi ili kuwawezesha kufanya tafiti na bunifu zitakazochochea mageuzi katika sekta ya kilimo.
“Wekezeni kwa wanasayansi chipukizi. Muwatajirishe kwa kuwawezesha kushiriki kwenye tafiti na bunifu mbalimbali,” amesema Dkt. Dongyu.
Ameongeza kuwa uzoefu wa Serbia unaonesha umuhimu wa kuwekeza kwa wataalamu na watafiti vijana, akisema hatua hiyo ilichangia mabadiliko na ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo.
Dkt. Dongyu pia amesisitiza umuhimu wa Serikali kuhakikisha wakulima wadogo wanashirikishwa katika maamuzi yanayohusu sekta ya kilimo, kwa kuwa wao ni miongoni mwa wadau wakuu na watekelezaji wa shughuli za kilimo.
Aidha, amesema FAO inaendelea kuhimiza matumizi ya viwango katika uzalishaji na biashara ya mazao, pamoja na matumizi ya teknolojia kuwaunganisha wakulima wadogo na masoko, hatua inayoweza kuongeza ushindani na kuwawezesha kunufaika na fursa za biashara.
Dkt. Mwigulu anamwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo wa kimataifa unaofanyika jijini Roma kuanzia Septemba 21 hadi 23, 2026.

