TANECU Yang'aza Korosho
Na. Wellu Mtaki, Dodoma
Sekta ya korosho nchini inaendelea kushuhudia mafanikio makubwa kutokana na ushirikiano imara kati ya Serikali na vyama vya ushirika, hatua inayochochea ongezeko la uzalishaji, kuimarisha masoko na kuongeza kipato cha wakulima katika maeneo mbalimbali yanayolima zao hilo.
Mafanikio hayo yameendelea kujidhihirisha kupitia maboresho ya mifumo ya biashara ya korosho, ambayo yameongeza uwazi, ufanisi na kuimarisha imani ya wakulima katika mnyororo mzima wa thamani wa zao hilo.
Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika Tandahimba na Newala (TANECU), Karim Hamis Chipola, alisema mageuzi yaliyofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa ushirika yamefungua ukurasa mpya wa maendeleo kwa wakulima wa korosho.
Alieleza kuwa matumizi ya mfumo wa stakabadhi za ghala, soko la bidhaa pamoja na vituo vya malipo yameongeza uwazi katika biashara ya korosho na kuhakikisha wakulima wanapata malipo yao kwa wakati, jambo lililozidi kuwapa ari ya kuongeza uzalishaji.
Chipola alisema TANECU imeanzisha vituo viwili vya malipo katika wilaya za Tandahimba na Newala, hatua iliyopunguza kwa kiwango kikubwa ucheleweshaji wa malipo na kutatua malalamiko yaliyokuwa yakijitokeza kwa wakulima katika misimu iliyopita.
Alibainisha kuwa chama hicho kinaendelea kuunga mkono kampeni ya "Linda Ushirika, Chagua Wadilifu", inayoratibiwa na Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha misingi ya uongozi bora ndani ya vyama vya ushirika.
Kwa mujibu wa Chipola, viongozi na wanachama wa Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) wanaendelea kupatiwa mafunzo ya uadilifu, usimamizi wa rasilimali na uwajibikaji, hatua inayolenga kujenga taasisi imara zitakazowanufaisha wakulima kwa muda mrefu.
Aidha, aliwahimiza wananchi na washiriki wa Maonesho ya Nanenane kutembelea banda la TANECU ili kujionea teknolojia za kisasa zinazotumika katika uzalishaji wa korosho, pamoja na kujifunza matumizi sahihi ya mizani ya kidijitali inayoongeza uwazi katika biashara.
Alisema banda hilo pia linatoa fursa ya kuona bidhaa mbalimbali za korosho zilizoongezwa thamani kupitia kiwanda cha TANECU, akisisitiza kuwa hatua hiyo inaonyesha dhamira ya chama hicho katika kukuza uchakataji wa mazao, kuongeza thamani ya korosho na kuinua uchumi wa wakulima pamoja na Taifa kwa ujumla.
