Breaking News

TADB YAPANUA HUDUMA YA UTOAJI WA MIKOPO

 

Na. Wellu Mtaki, Dodoma

WAZIRI Mkuu ameagiza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kuongeza uwezo wake wa kifedha pamoja na kupanua huduma za utoaji wa mikopo kwa lengo la kuwafikia wakulima, wafugaji na wavuvi wengi zaidi nchini. Amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza uwekezaji katika sekta za uzalishaji, kuharakisha mageuzi ya kilimo, mifugo na uvuvi, kuongeza tija na uzalishaji, sambamba na kuimarisha uchumi wa taifa kupitia sekta hizo zinazobeba maisha ya Watanzania wengi.

Akizungumza baada ya kutembelea banda la TADB katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea mkoani Dodoma, Waziri Mkuu amesema benki hiyo imeendelea kuwa chombo muhimu cha Serikali katika kuwezesha uwekezaji kwenye sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kwa kutoa mitaji kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wawekezaji mbalimbali.

Amesema ili Tanzania ifikie malengo ya kuongeza uzalishaji wa mazao na kuhakikisha usalama wa chakula nchini, kuna umuhimu wa kuendelea kuiwezesha TADB kifedha ili iweze kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya wakulima na wadau wengine wa sekta ya kilimo.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Serikali haiwezi kutegemea ruzuku pekee kila mwaka katika kuendeleza sekta ya kilimo, hivyo taasisi za kifedha kama TADB zina wajibu mkubwa wa kuhakikisha mitaji inapatikana kwa wakati kwa wakulima, wafugaji na wavuvi.

Amesisitiza kuwa benki hiyo inapaswa kuongeza uwezo wa kufadhili ununuzi wa mbolea, pembejeo, zana za kisasa za kilimo pamoja na miradi ya kuongeza thamani ya mazao ili kuongeza tija, ushindani na thamani ya bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Aidha, ameitaka TADB kushirikiana kwa karibu na Wizara za Kilimo na Mifugo pamoja na TAMISEMI kuwekeza katika miundombinu ya baada ya mavuno, hususan ujenzi wa maghala ya kuhifadhi mazao. Amesema hatua hiyo itaimarisha Mfumo wa Stakabadhi za Ghala na kuwawezesha wakulima kupata mikopo kwa kutumia mazao yao kama dhamana.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, Frank Nyabundege, amesema benki hiyo imeendelea kufadhili miradi mbalimbali ya kimkakati inayochochea ukuaji wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi nchini.

Amesema zaidi ya shilingi bilioni 700 zimetolewa kufadhili miradi ya umwagiliaji, huku zao la kahawa kutoka mikoa ya Kagera na Kigoma kupitia vyama vya ushirika likitajwa kuwa miongoni mwa mafanikio yaliyowavutia wadau wengi waliotembelea banda la TADB katika Maonesho ya Nanenane.

Nyabundege amesema TADB pia imewezesha mradi wa kisasa wa ufugaji na uchakataji wa samaki uliopo Bagamoyo unaotumia teknolojia kutoka Misri, wenye uwezo wa kuhifadhi hadi tani 90 za samaki kwa mwezi, huku ukizingatia uhifadhi wa mazingira na kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.

Ameeleza kuwa uwekezaji huo umechangia kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje, kuokoa fedha za kigeni, kuongeza ajira kwa Watanzania na kuimarisha mchango wa sekta za kilimo na uvuvi katika ukuaji wa uchumi wa taifa.