Breaking News

NIT YAONGEZA NGUVU UCHUKUZI

Na. Wellu Mtaki, Dodoma

Ukuaji wa uchumi wa Tanzania unaendelea kwenda sambamba na maendeleo makubwa ya sekta ya uchukuzi, jambo linaloongeza umuhimu wa kuwa na wataalamu wenye ujuzi wa kisasa wa kusimamia na kuendesha miundombinu hiyo. Kutokana na hali hiyo, Serikali imeendelea kuwekeza katika kuimarisha Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ili kiwe kitovu cha kuzalisha wataalamu watakaokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya sekta hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO, Mtumba, jijini Dodoma, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Mhandisi Dkt. Prosper Mgaya, alisema sekta ya uchukuzi ni miongoni mwa nguzo muhimu zinazochochea maendeleo ya uchumi wa taifa kwa kuwezesha usafirishaji wa watu na bidhaa kwa ufanisi.

Dkt. Mgaya alisema NIT imeendelea kupanua programu zake za mafunzo ili kuendana na ongezeko la mahitaji ya wataalamu katika sekta za usafiri wa barabara, reli, anga na majini. Alifafanua kuwa hatua hiyo inatokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya uchukuzi nchini.

Alieleza kuwa chuo hicho kilianzishwa mwaka 1975 kama kitengo cha Shirika la Usafirishaji la Taifa kabla ya kupandishwa hadhi mwaka 1982 na kuwa taasisi ya elimu ya juu yenye jukumu la kutoa mafunzo, kufanya tafiti pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu katika sekta ya uchukuzi.

Kwa mujibu wa Dkt. Mgaya, kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977 kulisababisha Tanzania kukumbwa na upungufu wa wataalamu wa sekta ya uchukuzi, hali iliyoifanya Serikali kuchukua hatua za kukiimarisha chuo hicho ili kiweze kuzalisha wataalamu wa kutosha kwa ajili ya mahitaji ya taifa

Alisema katika kipindi cha sasa, mahitaji ya wataalamu yameongezeka zaidi kutokana na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayoboresha mfumo wa uchukuzi nchini. Hivyo, NIT imeendelea kuboresha uwezo wake wa kufundisha ili kuhakikisha wahitimu wake wanakuwa tayari kukabiliana na changamoto za soko la ajira.

Aidha, alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika miradi mikubwa ya uchukuzi ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR), ununuzi wa ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), ujenzi na ukarabati wa meli pamoja na uboreshaji wa viwanja vya ndege, akisema miradi hiyo imefungua fursa nyingi za ajira na kuongeza mahitaji ya wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu.

Alisisitiza kuwa NIT itaendelea kuboresha mitaala yake kwa kuzingatia maendeleo ya teknolojia pamoja na kuimarisha mafunzo ya vitendo, hatua ambayo itawawezesha wahitimu wake kuwa na uwezo wa kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi

Dkt. Mgaya alihitimisha kwa kusema kuwa dhamira ya NIT ni kuendelea kuwa chuo kinachoongoza katika kuzalisha wataalamu wa sekta ya uchukuzi wenye weledi, ubunifu na uwezo wa kuchangia maendeleo endelevu ya uchumi wa Tanzania kupitia huduma bora za usafirishaji.