Breaking News

VETA Morogoro-Kihonda Yaja na Mashine ya Kisasa ya Kulimia Inayorahisisha Kilimo

 


Na Hawa Ismail, Dar es Salaam

Chuo cha VETA Morogoro-Kihonda kimewasilisha ubunifu wa mashine ya kisasa ya kulimia maarufu kama Pawatira, iliyobuniwa kwa kuzingatia mazingira halisi ya kilimo nchini ili kuwasaidia wakulima kuongeza ufanisi na kupunguza changamoto zinazowakabili mashambani.

Akizungumza leo katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mkufunzi Mwandamizi wa VETA Morogoro-Kihonda, Fredrick Uliki, alisema mashine hiyo imebuniwa baada ya kufanya utafiti wa kina kuhusu mashine zinazoagizwa kutoka nje, ambazo zimeonekana kutokidhi kikamilifu mazingira ya kilimo ya Tanzania.

"Tulibuni mashine hii kutokana na utafiti tulioufanya na kubaini kuwa baadhi ya mashine zinazoagizwa kutoka nje hazina uimara wa kutosha kufanya kazi kwa muda mrefu kwenye mashamba ya mabondeni na maeneo yenye milima. Hivyo tukaja na teknolojia inayokidhi mazingira yetu," alisema Uliki.

Alifafanua kuwa mashine hiyo imeundwa mahsusi kurahisisha kilimo cha mboga mboga, hususan kwa wakulima wanaolima katika maeneo ya mabondeni ambako matrekta makubwa hushindwa kufika kutokana na hali ya eneo.

"Mashine hii imebuniwa mahsusi kwa ajili ya kurahisisha kilimo cha mboga mboga, hasa kwa wakulima wa maeneo ya mabondeni. Tofauti na matrekta makubwa ambayo hupata ugumu kufika kwenye maeneo hayo, mashine hii inaweza kufanya kazi kwa urahisi na kuwasaidia wakulima kuongeza tija," alisisitiza Uliki

Aidha, alisema mashine hiyo pia ni muhimu kwa wakulima wa mpunga kwani husaidia kugandua ardhi na kulainisha udongo vizuri, jambo linalowezesha mbegu kuota kwa haraka na kwa wingi, hivyo kuongeza uzalishaji.

Uliki aliongeza kuwa uwezo wa mashine hiyo ni kulima hadi hekta tatu kwa siku, kutegemeana na nguvu ya mtumiaji, aina ya udongo pamoja na jiografia ya eneo husika.


 Alieleza kuwa maeneo tambarare huruhusu kazi kufanyika kwa kasi zaidi kuliko maeneo yenye miteremko au mabondeni.

Kwa upande wa matengenezo, alisema wakulima hawatapata changamoto ya upatikanaji wa vipuri kwani spea za mashine hiyo zinapatikana kwa urahisi katika mikoa mbalimbali nchini na zinauzwa kwa bei nafuu, hatua inayolenga kuhakikisha mashine hiyo inakuwa suluhisho endelevu kwa sekta ya kilimo.