TTCL Yaendelea Kung'ara Kibiashara, Yaleta Huduma Mpya za Kidijitali Sabasaba
Na Hawa Ismail- Dar es Salaam
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limesema linaendelea kuimarisha huduma za mawasiliano nchini kupitia matumizi ya Mkongo wa Taifa, huku likijivunia kuendelea kutengeneza faida baada ya kufanyiwa maboresho ya kiutendaji na kibiashara.
Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa, alisema shirika hilo linaonesha huduma mbalimbali za kidijitali zinazolenga kuharakisha safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kidijitali.
Alisema miongoni mwa huduma hizo ni intaneti ya kasi ya juu ya Supersonic Speed, kituo cha FTTX Experience Center kinachoonesha matumizi ya teknolojia ya nyumba janja (Smart Home), pamoja na huduma za cloud computing kupitia Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data (NIDC).
"Uchumi wa kidijitali hauwezi kufikiwa bila kuwa na mawasiliano ya uhakika na intaneti yenye kasi. Ndiyo maana tunaendelea kutumia Mkongo wa Taifa kuleta huduma bora na za gharama nafuu kwa Watanzania," alisema CPA Marwa.
Alifafanua kuwa teknolojia hizo zinawezesha matumizi mbalimbali ya kidijitali ikiwemo mifumo ya usalama wa nyumba, matumizi ya vifaa vya nyumbani kwa njia ya mtandao, michezo ya mtandaoni na huduma za video zenye ubora wa juu.
Kuhusu utendaji wa kifedha, Marwa alisema TTCL ilipata faida ya takribani shilingi bilioni 23 katika mwaka wa fedha 2024/2025, huku matokeo ya awali ya mwaka 2025/2026 yakionyesha kuwa mapato na faida vinaendelea kuongezeka.
Hata hivyo, alisema takwimu kamili za mwaka wa fedha uliohitimika hivi karibuni zitatangazwa baada ya kukaguliwa rasmi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Alisema mafanikio hayo yanatokana na maboresho ya kimkakati yaliyofanywa ndani ya shirika kufuatia maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha TTCL linaendeshwa kwa misingi ya kibiashara, ufanisi na faida.
![]() |

