Breaking News

DIB Yatumia Sabasaba Kuelimisha Umma Kuhusu Ulinzi wa Amana za Wateja

 


Na Hawa Ismail- Dar es Salaam 

Bodi ya Bima ya Amana (DIB) imeendelea kutumia Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mfumo wa bima ya amana, huku ikisisitiza umuhimu wa huduma hiyo katika kulinda amana za wateja wa benki na taasisi za fedha na kuimarisha imani katika sekta ya fedha nchini.

Msisitizo huo umejitokeza wakati Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Rahma Salim Mahfoudh, alipotembelea banda la DIB katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa, ambapo alipokelewa na viongozi pamoja na wafanyakazi wa Bodi hiyo na kupatiwa maelezo kuhusu majukumu yake, huduma inazotoa na kampeni za utoaji elimu kwa umma kuhusu Mfumo wa Bima ya Amana.

Akiwa katika banda hilo, Dkt. Mahfoudh alipata fursa ya kujionea mchango wa DIB katika kulinda amana za wateja wa benki na taasisi za fedha pamoja na kuimarisha uthabiti wa mfumo wa fedha nchini. Aliwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kutembelea maonesho hayo ili kujifunza huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi za umma na sekta binafsi.

"Ninawahimiza wananchi kutumia fursa hii kutembelea maonesho haya ili kujifunza mambo mbalimbali kutoka kwa taasisi na kampuni zinazoshiriki. Hapa kuna huduma, bidhaa, ubunifu na teknolojia zinazoweza kuongeza uelewa wao na kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi katika shughuli zao za kila siku," alisema Dkt. Mahfoudh.



Kwa upande wake, Afisa Mwandamizi wa DIB, Bi. Joyce Shala, alisema ushiriki wa Bodi hiyo katika Maonesho ya Sabasaba 2026 unalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu majukumu ya DIB katika kulinda amana za wateja wa benki na taasisi za fedha, pamoja na kuonesha umuhimu wa mfumo wa bima ya amana katika kudumisha utulivu na kuimarisha imani ya wananchi katika sekta ya fedha. Aidha, aliwataka wananchi kutembelea banda la DIB ili kupata elimu na ufafanuzi kuhusu huduma zinazotolewa na Bodi hiyo.