Breaking News

Diwani Makangarawe Amaliza Changamoto ya Madawati, Wanafunzi 300 Kunufaika

 


Diwani wa kata ya Makangarawe Fadhili Mboga akiongea na wazazi wa shule ya msingi Yombo Dovya 

Na Hawa Ismail- Dar es Salaam 

Diwani wa Kata ya Makangarawe, Fadhili Mboga, amemaliza changamoto ya upungufu wa madawati katika Shule za Msingi Yombo Dovya na Jitihada baada ya kukabidhi madawati 100 kwa shule hizo mbili.

Madawati hayo yalikabidhiwa leo Mei 16, 2026, katika kikao cha wazazi kilichofanyika shuleni hapo, ambapo diwani huyo alisema hatua hiyo imewaokoa wanafunzi zaidi ya 300 waliokuwa wakilazimika kukaa chini darasani huku akisisitiza kuwa ataendelea kufuatilia maendeleo ya elimu katika shule hizo.

“Maisha ya mwanafunzi yapo hapa shuleni, hivyo lazima tuhakikishe mazingira ya shule zetu yanakuwa salama na rafiki kwa watoto wetu,” alisema Mboga huku akiwashukuru wazazi kwa ushirikiano wao katika kutatua changamoto ya madawati.

Aidha, aliwataka wazazi kuendelea kushirikiana na walimu katika malezi ya watoto pamoja na kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na mahudhurio mazuri shuleni.

“Lazima tupambanie mahitaji ya msingi ya watoto wetu. Watoto wanashinda muda mwingi shuleni, hivyo tunapaswa kuhakikisha wanapata mazingira bora ya kujifunzia,” aliongeza Mboga.

Diwani huyo pia aliwahimiza wazazi kuwekeza zaidi kwenye elimu ya watoto wao akieleza kuwa elimu ni msingi wa mafanikio na husaidia kujenga maono ya maisha bora ya baadaye.

Mboga aliwashukuru wazazi wa Shule za Msingi Yombo Dovya na Jitihada kwa ushirikiano wao mkubwa katika kuunga mkono maendeleo ya shule hizo.

Katika hatua nyingine, diwani huyo alikabidhi vifaa vya michezo ikiwemo mipira na jezi kwa wanafunzi wa shule hizo, huku akisisitiza umuhimu wa michezo katika maendeleo ya watoto.

“Nakabidhi vifaa hivi vya michezo kwa watoto wetu, hivyo ni muhimu kuwepo ratiba nzuri ya michezo kwa ajili ya kuwajenga kiafya na kiushirikiano,” alisema Mboga

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Msingi Yombo Dovya, Salum Gawaza, aliwaomba wadau mbalimbali kuendelea kusaidia utoaji wa madawati na mahitaji mengine muhimu ili kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.

Naye Afisa Elimu wa Kata ya Makangarawe, Sophia Gindo, alimpongeza Diwani Mboga kwa juhudi zake kubwa za kuhakikisha wanafunzi wa Shule za Msingi Yombo Dovya na Jitihada wanapata madawati ya kutosha na kuondokana na changamoto ya kukaa chini darasani.