Breaking News

Diwani kata ya kivule Manyinya Azindua Kituo cha Bodaboda na Bajaji Bomba Mbili, Aahidi kutekeleza ahadi Nyingi kwa Vijana

 

Na Hawa Ismail-Dar es Salaam 

Diwani wa Kata ya Kivule, Rajabu Manyinya, amesema kuwa amejiandaa kikamilifu kutekeleza ahadi zote alizotoa kwa wananchi wa kata hiyo. Akizungumza katika uzinduzi wa kituo cha bodaboda na bajaji mtaa wa Bomba Mbili (Mwanzo Mgumu), diwani huyo aliwasilisha salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwapongeza wananchi kwa kutunza amani iliyopo.

Hafla hiyo imefanyika leo Januari 24, 2026, ambapo Manyinya alisema kuwa atahakikisha vijana wanapata bodaboda baada ya kukamilisha zoezi la usajili. Aidha, alitangaza kuwa tarehe 2 Januari 2026 kutafanyika zoezi la kuandikisha vitambulisho vya NIDA katika ofisi za Kata ya kivule ( misitu).

Diwani Manyinya alisisitiza kuwa wananchi wenye namba za NIDA lakini hawajapata vitambulisho watahakikishiwa kuvikabidhiwa, huku akieleza kuwa zoezi hilo litadumu kwa muda wa siku kumi.

Kuhusu huduma za afya, diwani huyo alisema kuwa dirisha la kujiunga na bima ya afya limefunguliwa, hususan kwa kundi la vijana. Alieleza kuwa mwanachama mmoja atachangia shilingi 40,000 kwa mwaka, huku kifurushi cha watu sita kikiwa ni shilingi 150,000. Aliongeza kuwa tayari ameshafanya mazungumzo na maafisa afya ili kuhakikisha wananchi wote wanasajiliwa kwenye bima hiyo.

“Dirisha la bima ya afya limefunguliwa. Vijana watachangia kiasi kidogo, na kama diwani wenu nimeshaongea na maafisa afya ili kila mmoja apate bima,” alisema Manyinya.

Pia alibainisha kuwa serikali italeta mpango maalumu wa kusajili kundi maalum litakalopata huduma za afya bila malipo, sambamba na huduma ya kuchukua miili ya marehemu bure.

Katika hatua nyingine, diwani huyo alikumbusha ahadi yake ya kujenga zahanati pamoja na shule mbili katika eneo la Bomba Mbili, ikiwemo shule ya sekondari na shule ya msingi, akiahidi kuzifungua na kuziboresha.

“Mmetengeneza banda zuri kwa upendo mkubwa, na hamjala hata fedha nilizochangia kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha bodaboda,” alisema Manyinya.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Bomba Mbili, Hassan Shamte, alisema kituo hicho cha bodaboda na bajaji kinaundwa na vijana watiifu na wenye nidhamu, hivyo aliwapongeza viongozi wa kijiwe hicho kwa ushupavu na uhimara wao.

Naye mlezi wa kijiwe cha Mwanzo Mwema alisema kuwa vijana hao wanaishi katika mazingira magumu na wanahitaji kushikwa mkono kwa kupewa fursa zitakazowawezesha kujikwamua kiuchumi.

Aidha, Mwenyekiti wa Kituo cha Bodabokda cha Bomba Mbili, Julius Mbwira, alisema kuwa kipaumbele cha kituo hicho ni nidhamu, akisisitiza kuwa hawaruhusu matumizi ya dawa za kulevya, lugha chafu wala wizi. Aliongeza kuwa baadhi ya vijana ni watiifu lakini hawana bodaboda, hivyo aliomba wasaidiwe. Alisema kwa sasa kituo hicho kina jumla ya wanachama 23 waliosajiliwa.