LAAC Yaanza Kuhoji Halmashauri 39 Nchini Rasmi
Na Wellu Mtaki, Dodoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeanza mchakato wa kuzipitia hoja za ukaguzi kwa kuzihoji halmashauri 39 kutoka mikoa 15 nchini, hatua inayolenga kuimarisha uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma na kuhakikisha hoja zote zilizobainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinapatiwa ufafanuzi na hatua stahiki.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha fedha zinazotolewa kwa halmashauri zinatumika kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa, huku ikiwataka viongozi wa halmashauri kuwajibika kikamilifu kwa dosari zilizoainishwa katika ukaguzi wa CAG.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Ado Shaibu Ado, ambaye pia ni Mbunge wa Tunduru Kaskazini, amesema zoezi hilo linafanyika baada ya Spika wa Bunge kutoa kibali kwa kamati kuendelea na uchambuzi wa hoja za ukaguzi zilizobaki baada ya Bunge la Bajeti.
Ameeleza kuwa wakati wa Bunge la Bajeti, kamati ilifanikiwa kuzihoji halmashauri nane pekee, lakini sasa imepewa nafasi ya kuendelea na halmashauri nyingine 39 kutoka mikoa 15 ili kuhakikisha hoja zote zinapatiwa ufafanuzi na hatua stahiki.
Kwa mujibu wa Ado, katika vikao hivyo kamati inawahoji Wakurugenzi wa Halmashauri ambao ni Maafisa Masuuli pamoja na timu zao za menejimenti, wakitakiwa kutoa majibu ya kina kuhusu hoja zote zilizobainishwa katika ripoti ya CAG kwa kila halmashauri husika.
Mbali na kusikiliza maelezo ya viongozi hao, kamati pia inafuatilia utekelezaji wa maagizo na maelekezo iliyowahi kuyatoa pamoja na mapendekezo ya CAG, kwa lengo la kujiridhisha kuwa mapungufu yaliyobainika yamefanyiwa kazi na hayajajirudia.
Ado amesema Kanuni ya 14 ya Kanuni za Kudumu za Bunge inaipa LAAC wajibu wa kwanza wa kuchunguza maeneo yote yenye matumizi mabaya ya fedha za Serikali za Mitaa yaliyobainishwa na CAG, kwa kuwahoji Maafisa Masuuli, kusikiliza utetezi wao na kutoa maelekezo ya awali pale inapohitajika.
Ameongeza kuwa jukumu la pili la kamati ni kufuatilia utekelezaji wa maagizo na mapendekezo yaliyotolewa na kamati yenyewe pamoja na yale ya CAG, ili kuhakikisha kasoro zilizobainishwa zinarekebishwa kwa wakati na haziendelei kujitokeza katika halmashauri.
Aidha, amesema jukumu la tatu ni kuishauri Serikali na mamlaka za Serikali za Mitaa kuhusu njia bora za kuimarisha usimamizi wa fedha za umma, kuongeza uwajibikaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kupitia matumizi yenye tija ya rasilimali za umma.
Ado amesema baada ya kukamilika kwa zoezi la kuhoji halmashauri zote 39, kamati itaandaa taarifa yenye uchambuzi na mapendekezo yatakayowasilishwa bungeni kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa kuwa maazimio rasmi ya Bunge, yatakayokuwa maelekezo kwa Serikali kuhusu hatua za kuchukua.


