Serikali Yaendelea Kuimarisha Haki, Usawa Mitihani ya Taifa
Na Wellu Mtaki -Dodoma
Waziri wa Elimu, Sayansi, na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema serikali inaendelea kuimarisha haki na usawa katika mitihani ya kitaifa ya kidato cha sita na vyuo vya ualimu.
Akizungumza Mei 7, 2026 jijini Dodoma, Prof. Mkenda amesema serikali inaimarisha zoezi hilo la upimaji kwa kuweka usimamizi imara katika mitihani hiyo.
"Hatupendi kupoteza mtu yeyote katika mitihani hii, lakini yeyote atakayekiuka kanuni tutamchukulia hatua," alionya.
Kauli ya Waziri Mkenda imekuja kufuatia uwepo wa uvumi kwamba baadhi ya shule zinazomilikiwa na wanasiasa ambazo wanasoma watoto wa matajiri huvujishiwa mitihani kutokana na wazazi wao kutoa hongo.
Uvumi huo husababisha minung'uniko miongoni mwa watoto wa kimasikini hali inayoonesha kuwa mfumo wa elimu umegubikwa na hali ya kutokuwa na haki na usawa ambayo inaligawa Taifa kati ya wenye nacho na wasiokuwa nacho.
Waziri Mkenda amesema wanafunzi 133,655 wa kidato cha sita na walimu 14,679 wameanza mitihani yao ya kuhitimu elimu zao.
