Asilimia 56 ya Wanawake Wapinga Unyanyasaji
Na Wellu Mtaki - Dodoma
Asilimia 56 ya wanawake wote nchini Tanzania wanakataa aina zote za unyanyasaji.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima katika uzinduzi wa matokeo ya tafiti mbili zilizofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Mei 6, 2026 jijini Dodoma.
NBS imefanya utafiti huo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Benki ya Dunia, Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO), na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake (UN Women).
"Matokeo ya tafiti hizo kwenye uhuru na haki zinaonesha kuwa asilimia 26 tu ya Wanawake nchini Tanzania wanaamini wanawake Wanapaswa kuwa na haki ya kufanya maamuzi kuhusu njia za kujikimu kimaisha,huku asilimia 34 ya Wanawake wanaunga mkono haki ya Wanawake kuhusu ndoa, talaka na kupata watoto na asilimia 56 ya Wanawake wanakataa aina zote za unyanyasaji," alisema.
Kwa upande wake, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau katika uzalishaji wa takwimu sahihi na za kuaminika.
Alisema lengo ni kuhakikisha takwimu hizo zinasambaa ili zitumike ipasavyo katika kupanga sera na mipango ya maendeleo.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Takwimu na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda, ametoa wito kwa taasisi za umma na binafsi kutumia kikamilifu takwimu hizo katika kufanya maamuzi sahihi.
Tafiti hizo ambazo zimezinduliwa ni pamoja na Utafiti wa uwezeshwaji wanawake na lishe wa mwaka wa Kilimo 2023/2024, na Utafiti wa Mazingira na jinsia wa mwaka 2025 ambapo kwa pamoja zinalenga Kuchochea mabadiliko mbalimbali yakiwemo ya kiuchumi.


