Breaking News

WAZIRI MKUU ATARAJIWA KUFANYA ZIARA MKOANI DODOMA

 




Na. Wellu Mtaki, Dodoma 

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amewataarifu wananchi wa Dodoma na Watanzania kwa ujumla kuwa, Aprili 12, 2026, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Lameck Nchemba, anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Chamwino, Jimbo la Mvumi 

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 10, 2026 jijini Dodoma, Senyamule amesema kuwa lengo la ziara hiyo ni kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kuzungumza na wananchi, kusikiliza changamoto zao, pamoja na kutoa maelekezo ya Serikali kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma na maendeleo katika maeneo husika.

Ameongeza kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma inawaomba wananchi wa Wilaya za Bahi na Chamwino kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mapokezi na mikutano itakayofanyika wakati wa ziara hiyo, ili kupata fursa ya kuwasilisha kero na maoni yao moja kwa moja kwa Waziri Mkuu.

Aidha, amewahimiza wananchi kuendelea kudumisha amani, utulivu na ushirikiano katika kipindi chote cha ziara hiyo, ili kuendelea kuuenzi na kuufanya Mkoa wa Dodoma kuwa fahari ya Watanzania.