CCM IMEWAONYA WANASIASA KUSEMA UONGO KUHUSU ONGEZEKO LA BEI LA MAFUTA
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi, amewataka baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kuacha kupotosha wananchi kwa kutoa taarifa zisizo sahihi kuhusu hali ya mafut nchini.
Kihongosi ameyasema hayo leo Aprili 7, 2026 jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambapo alieleza kuwa sababu kuu ya kuongezeka kwa bei ya mafuta ni kufungwa kwa mkondo wa bahari inayotumika kusafirisha mafuta kutoka Mashariki ya Kati kuja Afrika Mashariki.
“Ni lazima tufahamu kuwa njia hiyo ya bahari hubeba takribani asilimia 20 ya mafuta duniani. Kufungwa kwake kuna athari ya moja kwa moja, ikiwemo kupanda kwa bei ya mafuta hapa nchini,” amesema Kihongosi.
Amefafanua kuwa hali hiyo imesababisha bei ya mafuta katika soko la dunia kupanda kwa kiasi kikubwa, kutoka dola za Marekani 700–800 hadi kufikia dola 1,700–1,800. Ongezeko hilo limeathiri pia bei za ndani kwa kupanda kwa zaidi ya shilingi 800 hadi 1,000 kwa lita.
Aidha, alieleza kuwa gharama ya “premium” imeongezeka kutoka dola 80–110 hadi kufikia dola 270–300, hali iliyochangia ongezeko la zaidi ya shilingi 200 kwa lita, na kufanya jumla ya ongezeko kufikia zaidi ya shilingi 1,000.
Wakati huohuo, Kihongosi alitaja hali ya bei za mafuta katika baadhi ya nchi, akieleza kuwa Zimbabwe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Afrika Kusini bei imefikia takribani shilingi 5,000 kwa lita. Nchini Kenya, bei iko kati ya shilingi 3,500 hadi 4,000 kwa lita.
Aliongeza kuwa changamoto ya uhaba wa mafuta si Afrika pekee, bali pia imeathiri Ulaya na Asia, akitolea mfano Uswisi ambapo bei ni kati ya shilingi 5,000 hadi 6,000 kwa lita, na Uingereza kati ya shilingi 5,500 hadi 6,500 kwa lita.
Kutokana na hali hiyo, CCM imeishauri serikali kuangalia uwezekano wa kutoa ruzuku ili kupunguza makali ya bei kwa wananchi. Kihongosi alisisitiza kuwa chama hicho pamoja na serikali yake vitaendelea kuhakikisha upatikanaji wa mafuta nchini unakuwa wa uhakika.
Aidha, chama hicho kimeitaka wizara husika kuimarisha upatikanaji wa mafuta, huku Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) likitajwa kuwa kiungo muhimu katika uagizaji wa mafuta na kudhibiti vitendo vya hujuma, ikiwemo uchepushaji wa meli za mafuta kwa maslahi binafsi.
“Tunapongeza juhudi za TPDC. Licha ya baadhi ya nchi kukosa mafuta, Tanzania inaendelea kuwa na uhakika wa nishati hiyo. Serikali imekuwa makini kukabiliana na changamoto hii, ikiwa ni pamoja na hatua ya kutoa ruzuku mwaka 2022 chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema Kihongosi.
Vilevile, CCM imeitaka serikali kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza utegemezi wa mafuta, hususan katika taasisi za umma na binafsi. Hii ni pamoja na matumizi ya gesi asilia kwenye magari, bajaji, mitambo na vyombo vingine vya usafiri.
Kwa upande mwingine, chama hicho kimependekeza kuanzishwa kwa mfuko maalumu wa kukabiliana na changamoto za mafuta, pamoja na kuwekeza katika ujenzi wa hifadhi kubwa za mafuta ili kuhakikisha nchi inakuwa na akiba ya kutosha nyakati za dharura.
