Jamii Yahimizwa Kuwajali na kuwakumbuka Watoto wa wenye mahitaji maalum Katika makao ya Taifa ya kulelea Watoto Kikombo- Dodoma
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Meneja wa Makao ya Taifa ya kulelea Watoto Kikombo, Darius Kalijongo, ametoa wito kwa jamii kuwakumbuka na kuwajali watoto wa wenye mahitaji maalumu kwa kuwapatia malezi bora, akisisitiza kuwa watoto hao wanapaswa kulelewa katika mazingira ya familia yenye upendo na ulinzi.
Kalijongo ameyasema hayo Aprili 11, 2026 jijini Dodoma katika kituo hicho, akielekea maadhimisho ya Siku ya Watoto wa Mtaani Duniani yanayofanyika kila mwaka Aprili 12.
Amesema watoto hao ni sehemu ya jamii hivyo wanastahili kupewa nafasi ya kuonekana, kuthaminiwa na kusaidiwa.
Ameeleza kuwa kituo hicho kimebeba jukumu la wazazi kwa kuhakikisha watoto wanapatiwa huduma zote za msingi ikiwemo elimu, afya, chakula na malezi, pamoja na kuwajengea uwezo wa kujitambua kupitia shughuli mbalimbali kama kilimo, bustani, usafi wa mazingira na huduma za kiroho.
“Ni kweli zipo changamoto kutokana na malezi wanayoyapitia watoto hawa, lakini kupitia wataalamu wa ustawi wa jamii tulionao, tunatumia elimu na uzoefu wetu kuhakikisha tunawarejesha watoto katika mstari sahihi,” amesema Kalijongo.
Aidha, ametoa wito kwa jamii, taasisi za kidini, wanasiasa na wanahabari kujitokeza kusaidia kituo hicho kwa kutoa mahitaji mbalimbali pamoja na kukitangaza ili kuongeza uelewa kwa jamii.
Amesema kituo kina uwezo wa kuhudumia watoto 250 kwa wakati mmoja, lakini kwa sasa kinahudumia watoto 197, wakiwemo wavulana 104 na wasichana 93.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kikombo, Emmanuel Alex Manyono, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kujenga kituo hicho na kuendelea kutoa msaada kwa watoto hao.
Amesema uwepo wa wadau mbalimbali wanaotembelea kituo hicho na kutoa misaada ikiwemo nguo, madaftari, vyakula na mahitaji mengine, ni ishara ya upendo na mshikamano kwa watoto wenye uhitaji.
“Tunatoa wito kwa mashirika, vikundi na watu binafsi kuendelea kufika hapa, kushirikiana na watoto hawa na hata kula nao chakula, ili wajione kuwa ni sehemu ya jamii,” amesema Manyono.
Naye mmoja wa watoto wanaoishi katika Makao ya Taifa ya Kikombo ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha kupata elimu na ujuzi mbalimbali.
Watoto hao wamesema wamefaidika kwa kupata mahitaji muhimu kama elimu, malazi na chakula, pamoja na mafunzo ya ujuzi wa maisha ikiwemo upishi, kilimo, ushonaji na ufugaji. Aidha, wamepongeza juhudi za serikali za kuwawezesha kuendelea na mafunzo ya ufundi stadi (VETA) ili kutimiza ndoto zao za maisha.





