RAIS SAMIA AWAAGIZA WIZARA 5 KUINUA MAMA NA BABA LISHE
Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amezielekeza wizara tano muhimu kuchukua hatua za haraka kuboresha ustawi wa mama na baba lishe nchini, akiwatambua kama nguzo muhimu ya ajira na uchumi.
Akizungumza Aprili 21, 2026 jijini Dar es Salaam katika Mkutano wa Kitaifa wa Lishe, Rais Samia alizitaka Wizara za Fedha, Afya, Nishati, Maendeleo ya Jamii pamoja na Wizara ya Habari na Teknolojia ya Habari kushirikiana na TAMISEMI kuhakikisha kundi hilo linapata mazingira bora ya kazi, heshima na ulinzi dhidi ya unyanyasaji.
Aidha, alisisitiza upatikanaji wa mikopo na mafunzo kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na taasisi za kifedha, huku TAMISEMI ikitakiwa kuandaa maeneo rasmi ya biashara yenye miundombinu rafiki. Pia Wizara ya Afya imeagizwa kuboresha huduma za afya na kuhamasisha kujiunga na bima kupitia NHIF.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa Mama Lishe Tanzania (UMALITA), Havijawa Omary, alimshukuru Rais Samia kwa kuwapa heshima mama na baba lishe kupitia ushiriki wake kwenye kongamano hilo, akisisitiza kuwa sekta hiyo inaweza kuitangaza Tanzania kupitia utalii wa vyakula.
Havijawa alisema UMALITA imejipanga kuanzisha matamasha na kampeni mbalimbali ikiwemo “Pilau la Mama Samia” na mbio za UMALITA, pamoja na kuhamasisha matumizi ya vyakula vya asili kama mrenda, makande na michende. Pia aliwataka wanawake kujiunga na chama hicho ili kunufaika na fursa za mikopo, mafunzo na bima ya afya.





