Breaking News

MIGOGORO YA ARDHI YAWAIBUA WANASHERIA

 


Na,  Wellu Mtaki- Dodoma

Njia ya kutatua migogoro ya ardhi uliopo katika takriban halmashauri zote nchini ni moja ya mada zilizojadiliwa katika mdahalo wa wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo vya kati katika Ukumbi wa Chimwaga uliopo katika Chuo Kikuu cha Dodoma Aprili 27, 2026.

Mdahalo huo uliojadili nafasi ya vijana katika kuchochea huduma za kisheria nchini, ulihudhuriwa na takriban wanafunzi 2000 wa Chuo Kikuu cha Dodoma, wakufunzi wa sheria kutoka vyuo mbalimbali, wanasheria, na wanahabari.

Mgeni Rasmi katika Mdahalo huo, Mkurugenzi wa Msaada wa Huduma za Kisheria wa Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Esther Msambazi amesema serikali inasimamia zaidi ya vituo 100 vya msaada wa kisheria nchi nzima ili kuwawezesha wananchi kupata msaada wa kisheria jambo litakalotokomeza dhulma na uonevu nchini.

Mkurugenzi wa Kliniki ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dodoma, ambaye pia ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza chuoni hapo, Bw. Eliah Rushongo alisema wanafunzi chuoni hapo wanatoa msaada wa kisheria kwa wananchi wote bila malipo.

Katika mdahalo huo, wanafunzi wa UDOM walionesha igizo lenye maudhui ya migogoro ya ardhi, jinsi wenye uwezo wanavyotumia fedha zao kudhulumu ardhi na kuwatishia wamiliki, na namna msaada wa sheria unavyoweza kulinda haki ya watu wa vipato vya chini.

Amidi wa Shule Kuu ya Sheria ya UDOM, Dkt. Elia Mwanga aliishukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuandaa mdahalo huo ambao unawapa fursa wanafunzi katika kutatua matatizo mbalimbali yanayoikabili jamii.

Naye, Mkurugenzi wa TEHAMA Mahakama Kuu, Bw. Kalege Enock alitoa wito kwa vijana kuandaa ubunifu wa mifumo ya kimtandao itakayowawezesha wananchi kujifunza sheria na kupata msaada wa kisheria popote walipo.

Wizara ya Katiba na Sheria inaendesha midahalo katika vyuo vikuu na vyuo vya kati mbalimbali nchini ili kuwawezesha vijana kutoa msaada wa kisheria pindi watakapohitimu masomo yao.