NBC Yatoa Milioni 150 Kufadhili Mafunzo ya Ufundi stadi VETA kwa Vijana 588
Na Mwandishi Wetu- Dar es Salaam
Benki ya NBC imetoa jumla ya shilingi milioni 150 kufadhili mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana 588 kupitia mpango wake maalum unaojulikana kama “NBC Wajibika Scholarship,” hatua inayolenga kuongeza ujuzi na ajira kwa vijana nchini. Uzinduzi wa mpango huo umefanyika jijini Dar es Salaam, ukianza na mikoa ya Morogoro na Mwanza kutokana na uhitaji mkubwa wa mafunzo ya ufundi katika maeneo hayo.
Akizungumza Aprili 21, 2026 wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi, amesema benki hiyo inaunga mkono juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana. Amesema zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wana umri chini ya miaka 35, huku kila mwaka vijana kati ya laki nane hadi milioni moja wakiingia katika soko la ajira bila kuwa na ujuzi unaohitajika.
Sabi amesema hali hiyo imekuwa ikisababisha ongezeko la ajira zisizo na tija na wakati mwingine kuwaingiza vijana katika vitendo visivyofaa.
Amesisitiza kuwa mpango huo unalenga kuwajengea vijana ujuzi wa vitendo utakaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa katika sekta mbalimbali za uchumi.
"Mafunzo hayo yatadumu kati ya miezi mitatu hadi sita na yatatolewa katika vituo vya VETA vilivyopo Morogoro na Mwanza. Aidha, washiriki wote watafunguliwa akaunti za NBC KuaNasi ili kuwawezesha kupata huduma rasmi za kifedha na kujenga msingi imara wa kiuchumi" amesema Sabi
Kwa mujibu wa Sabi, fani zitakazotolewa zimezingatia mahitaji ya soko la ajira, zikiwemo ufundi umeme, uhandisi mitambo, ujenzi pamoja na huduma za hoteli na utalii.
Pia, kupitia majukwaa ya NBC Business Club, wahitimu watapatiwa elimu ya fedha pamoja na fursa za mitaji na uwekezaji ili kukuza shughuli zao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Antony Kasore, amesema vigezo vya kujiunga na mafunzo hayo ni pamoja na uwezo wa kusoma na kuandika, umri unaokidhi masharti pamoja na kufaulu katika mchakato wa uchambuzi wa waombaji.
Ameongeza kuwa mpango huo ni wa awamu ya kwanza, na awamu nyingine zitaendelea ili kuwapa nafasi zaidi vijana watakaokosa katika hatua ya mwanzo.
Kasore amesema VETA imejipanga kutoa mafunzo kwa vijana 120,000 kila mwaka, ambapo hadi sasa vijana zaidi ya 101,000 wameshafikiwa. Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya vyuo vya ufundi, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vyuo 65 katika wilaya mbalimbali, ili kuhakikisha mafunzo yanawafikia Watanzania wengi zaidi karibu na maeneo yao.