TAKUKURU TEMEKE YAMFIKISHA ASKOFU MAHAKAMANI KWA TUHUMA ZA KUGHUSHI NYARAKA ZA ARDHI
Na Mwandishi Wetu- Dar es Salaam
Naibu mkuu wa TAKUKURU Temeke Ismail Bukuku amesema katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2025, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke imefanikisha kumfikisha mahakamani Askofu Renatus Joseph Nyalali, Askofu kutoka kanisa la Hosanna Assemblies of God Tanzania (HAOGT), kwa tuhuma za kughushi nyaraka na kutoa nyaraka za uongo zinazohusiana na umiliki wa ardhi.
Ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam Machi 5,2026 wakati alipozungumza na waandishi wa habari amabapo Ismail Bukuku alisema lengo la askofu huyo ili aweze kupata kiwanja chenye thamani ya milioni 60,000,000
"Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia uchunguzi wa kina uliofanywa na TAKUKURU, baada ya kupokea taarifa kutoka kwa mmoja wa warithi na msimamizi wa mirathi ya marehemu Ally Hamad Hillal" amesema Bukuku
Hata hivyo Bukuku alisema kutokana na ushahidi uliokusanywa na kufanyiwa uchambuzi wa kitaalamu, TAKUKURU imefungua kesi ya jinai namba CC/26097/2025 dhidi ya Askofu Renatus Joseph Nyalali, katika Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni.
Katika hatua nyingine alisisitiza kuwa kwa Mujibu wa hati ya mashtaka, imedaiwa kuwa katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2022, mshtakiwa alighushi nyaraka na sahihi za wanafamilia wa marehemu kwa lengo la kujipatia umiliki wa eneo la ardhi lililopo Mtaa wa Kizani, Geza Ulole, Wilaya ya Kigamboni.
Eneo hilo lilinunuliwa mwaka 2008 kwa kiasi cha shilingi milioni sitini na kuachwa kama urithi kwa watoto wa marehemu
Hata hivyo Bukuku alitoa wito kwa wananchi wa Wilaya za Temeke na Kigamboni aliwahimiza kwa dhati kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa ambapo alisema vita hii si ya taasisi moja pekee, bali ni jukumu la kila mmoja wetu kwa mshikamano, ujasiri na uwajibikaji wa pamoja ndipo tutaweza kujenga Tanzania yenye haki, uadilifu na maendeleo ya kweli, Tanzania isiyokuwa na rushwa.
Tujiepushe kabisa na vitendo vya rushwa kwa namna yoyote ile, na kuchukua hatua za kijasiri kwa kutoa taarifa pale wanapobaini dalili za rushwa katika maeneo yao.
Bukuku alisema serikali imeweka mifumo salama ya kupokea taarifa, ikiwemo Ofisi za TAKUKURU zilizo karibu na wananchi pamoja na namba ya simu 113, ambayo ni bure na inapatikana muda wote
