ALHIKMA FOUNDATION YATOA SHUKRANI KWA WALIOFANIKISHA MASHINDANO YA QURAN
Na Hawa Ismail- Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Alhikma Foundation na wa Mashindano Makubwa ya Qurani Tukufu ya Mabara Yote Duniani Nurdin Kishki amesema taasisi hiyo imeandaa tukio maalum la kutoa shukrani kwa watu mbalimbali waliotoa mchango wao kufanikisha mashindano ya mwaka 2026. Amesema tukio hilo ni la kuthamini juhudi za wadau na wajitolea waliosaidia kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika kwa mafanikio.
Amesema hayo leo jijini Dar es Salaam March 5,2026 wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari amabapo alisema Taasisi ya Alhikma Foundation si taasisi ya kidini pekee bali pia ni taasisi ya kijamii inayoshirikisha wadau mbalimbali. Kwa mujibu wake, mafanikio ya mashindano hayo yametokana na ushirikiano wa watu wengi kwa kuwa kazi kubwa kama hiyo haiwezi kufanywa na mtu mmoja.
Mwenyekiti huyo alibainisha kuwa zaidi ya vijana na watu wazima 1,221 walijitolea kama volunteers kusaidia maandalizi na uendeshaji wa mashindano hayo yaliyofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. Alisema wengi wao walifanya kazi hiyo bila malipo kwa mapenzi yao kwa Qurani Tukufu.
"Miongoni waliozawadiwa zawadi pamoja na Snura Mushi Tiketi mbili za kwenda kuhiji Makka, Issa Makungu Tiketi moja kwenda kuhiji Makka, Seif Abdallah Tiketi moja kwenda kuhiji Makka, Idd Kazumari amezawadiwa shilingi 500000 na simu ya mkononi, Pamoja na Mwalimu Yassini Ally amezawadiwa shilingi 500000 na simu ya mkononi" alikabidi Kishki
Aidha Mwenyekiti huyo alitoa shukrani kwa Waislamu na Watanzania waliokusanyika kwa wingi uwanjani licha ya changamoto ya mvua kubwa iliyonyesha siku ya mashindano. Alisema hali hiyo ilionyesha imani na mapenzi makubwa ya watu kwa Qurani Tukufu.
Pia Kishki aliwashukuru waandishi wa habari na vyombo vya habari kwa kuripoti tukio hilo kupitia televisheni, mitandao ya kijamii na majukwaa mbalimbali ya habari. Alisema mchango wao umewezesha mashindano hayo kufuatiliwa na watu wengi ndani na nje ya nchi.
Katika hafla hiyo, baadhi ya wajitolea waliotumia muda na nguvu zao katika mashindano hayo walitambuliwa na kupewa zawadi mbalimbali ikiwa ni ishara ya shukrani kwa mchango wao.
Mwenyekiti huyo alihitimisha kwa kuwatakia baraka na kheri wote waliochangia kufanikisha mashindano hayo, akisisitiza kuwa taasisi hiyo itaendelea kuhamasisha jamii kuthamini na kusoma Qurani Tukufu.








