Ngome ya Wanawake ACT-Wazalendo Yasitisha Sherehe za Siku ya Wanawake Duniani, Yatangaza Maombolezo ya Kitaifa
Na Mwandishi Wetu
NGOME ya Wanawake ya ACT-Wazalendo imetangaza kuwa haitasherehekea Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu, badala yake itaitumia siku hiyo kuomboleza kufuatia vifo na ulemavu wa kudumu uliowakumba baadhi ya Watanzania wakati wa ghasia zilizotokea Oktoba 29, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari Februari 26, 2026 katika Makao Makuu ya chama hicho yaliyopo Magomeni jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake, Janeth Rithe, amesema hawana sababu ya kusherehekea siku hiyo wakati bado mioyo ya Watanzania inaendelea kuumizwa na majonzi ya kupoteza wapendwa wao, huku wengine wakibaki na ulemavu wa kudumu.
Amesema kuwa mwezi mzima wa Machi utakuwa ni mwezi wa maombolezo, kwa lengo la kuwakumbuka wanachama wa chama hicho na Watanzania kwa ujumla, pamoja na kuonesha mshikamano na familia zote zilizoathirika na matukio hayo.
Aidha, Rithe amesema kuwa Machi 8, 2026, Ngome ya Wanawake itaandaa shughuli mbalimbali ikiwemo kufanya maombi na hitma, kutembelea wazee na watoto yatima, kufanya usafi katika vituo vya afya, kutoa misaada, kuchangia damu, kuzuru makaburi pamoja na kufanya mikutano mikubwa ya hadhara kote nchini.
Ameongeza kuwa maombolezo hayo yataendeshwa chini ya kauli mbiu isemayo “Machozi ya Mama ni Deni la Taifa,” akisisitiza kuwa ni wajibu wa jamii na Taifa kwa ujumla kutambua na kuguswa na maumivu yanayowakumba wanawake na familia zilizoathirika.
