WALICHOSHTAKI WAUMINI WAKATOLIKI KWA PAPA DHIDI YA RUWA’ICHI NA KITIMA HIKI HAPA*
Na. Mwandishi wetu,
Jana, waumini wa Kanisa Katoliki zaidi ya 100 walishuhudiwa wakigonga hodi katika Ubalozi wa Vatican nchini Tanzania kukabidhi barua ya madai (petition) dhidi ya Askofu Jude Thaddeus Ruwa’ichi, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, na Padri Charles Kitima, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.
Chumba chetu cha habari kimeinasa barua hiyo ambayo kimsingi ni malalamiko ya kikanisa (formal canonical petition) yaliyowasilishwa kwa Papa kupitia Ubalozi wa Vatican Tanzania, yakirejea madai mahsusi dhidi ya kila mmoja wa viongozi hao wa Kanisa.
*Walichomshtaki Padri Charles Kitima*
Kwa mujibu wa barua hiyo, waumini wanamshutumu Padri Kitima kwa:
•Kujihusisha na masuala ya siasa kwa upendeleo, wakidai kauli na mienendo yake ya hadharani imekuwa ikitafsiriwa kama kuunga mkono upande mmoja wa kisiasa(CHADEMA), hali inayokiuka msimamo wa Kanisa wa kutobagua kisiasa.
•Kulisababishia Kanisa mgawanyiko na skendo, kwa kauli zinazodaiwa kuwachanganya waumini na kulifanya Kanisa lionekane mshiriki wa mvutano wa kisiasa.
•Kukiuka wajibu wa kichungaji, kwa kushindwa kulinda umoja, amani na uaminifu wa waumini kama inavyotakiwa na Sheria za Kanisa (Canon Law).
Waumini wanaiomba Vatican ichunguze mwenendo wake kwa lengo la kurejesha uadilifu, tahadhari ya kichungaji na uaminifu wa Kanisa mbele ya waumini na jamii.
*Walichomshtaki Askofu Jude Thaddeus Ruwa’ichi*
Dhidi ya Askofu Ruwa’ichi, barua inaeleza madai mazito zaidi yakihusisha:
•Matumizi ya lugha ya kudhalilisha na ya matusi dhidi ya waumini waliotumia haki yao ya kumuandikia Papa, lugha inayodaiwa ilitumiwa hadharani wakati wa ibada.
•Kuwaaibisha na kuwavunjia heshima waumini kutoka madhabahuni, hatua ambayo waumini wanasema ilizalisha hofu, maumivu ya kisaikolojia na kuwanyima ujasiri wa kutumia haki zao za kikanisa.
•Kukiuka Sheria za Kanisa (Canon Law) zinazolinda heshima na sifa njema ya waumini, na zinazomtaka askofu awe kielelezo cha unyenyekevu, upole na ulinzi wa kondoo wa Kristo.
•Kuvunja mafundisho ya Biblia na Mapapa, yanayokataza lugha ya kejeli, dharau na hukumu dhidi ya waumini, hasa katika ibada za hadharani.
Kwa mujibu wa barua hiyo, matendo hayo yamesababisha skendo, mgawanyiko na kuporomoka kwa imani ya waumini kwa baadhi ya viongozi wao wa juu wa Kanisa.
*Ombi kwa Papa*
Katika hitimisho lao, waumini wanamuomba Papa:
•Ayapokee na kuyachunguza madai yote kwa kina;
•Achukue hatua stahiki za kikanisa dhidi ya wahusika;
•Alinde heshima ya waumini, umoja wa Kanisa na uaminifu wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania.
Aidha, waumini hao wanasema hatua yao si uasi bali ni matumizi halali ya haki yao ya kikanisa, wakisisitiza kuwa lengo lao ni kulilinda Kanisa, si kulidhoofisha.
Zaidi soma barua hiyo hapa
