Mamlaka ya mafunzo ya amali ( VTA) -Yajizatiti Kuinua Ujuzi wa Vijana kwa Mafunzo ya Ufundi Stadi
Na Mwandishi Wetu- Zanzibar
Katika juhudi za kuhakikisha upatikanaji wa ujuzi wa ufundi stadi visiwani Zanzibar, Mamlaka ya mafunzo ya amali (VTA)- kimejipanga kukuza vipaji na ubunifu wa wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali vya nchini kwa kushirikiana na vyuovya ufundi stadi VETA. Lengo kuu ni kuhakikisha vijana wanapata elimu ya vitendo itakayowawezesha kukidhi mahitaji ya soko la ajira na kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Akizungumza katika maonyesho ya wafanyabiashara yanayoendelea Zanzibar, Afisa Masoko wa Kampuni ya Ujuzi VETA, Bi. Janeth Nkondora, alieleza kuwa mafunzo ya ufundi stadi ni njia bora ya kujipatia kipato kwa mtu mmoja mmoja na kuinua pato la taifa kwa ujumla. Alisisitiza umuhimu wa vijana kujiunga na mafunzo hayo ili kujenga msingi imara wa maisha yao ya baadaye.
"Ujuzi wa vitendo unaotolewa kupitia VTA unamwezesha mhitimu kuwa tayari kwa ajira au kujiajiri, jambo ambalo ni muhimu sana katika kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira," alisema Bi. Nkondora.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Bw. Abdallah Mohamed, aliipongeza VTA kwa ubunifu wake na mchango wake katika maendeleo ya vijana. Aliwahimiza vijana kujitokeza kwa wingi kujiunga na mafunzo hayo, akisema kuwa ni fursa ya kipekee ya kujijengea maisha bora.
Ikumbukwe kuwa VTA- imeweka mikakati madhubuti ya kuwawezesha vijana kujiajiri na kuongeza uzalishaji katika jamii, hatua inayolenga kuleta maendeleo endelevu kwa taifa.



