Katibu Mkuu Jumuiya ya Wafanya Biashara Aipongeza VETA kwa kutoa Mafunzo ya Ufundi Stadi
Na Mwandishi Wetu
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wafanya Biashara Tanzania, Abdallah Mohamed, amepongeza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa kazi kubwa inayofanya katika kutoa mafunzo ya ufundi stadi nchini.
Pongezi hizo amezitoa leo, Januari 6 2026, alipotembelea banda la VETA lililopo katika Viwanja vya Dimani, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar, wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Biashara Zanzibar (ZITF).
Maonesho hayo yameanza Desemba 29, mwaka jana 2025 na yanatarajiwa kuhitimishwa Januari 16, mwaka huu 2026.
Akiwa katika banda hilo, Mohamed amepatiwa maelezo kuhusu namna VETA inavyotoa mafunzo ya ufundi stadi pamoja na taarifa za mchango wa walimu, wahitimu na wanafunzi mahiri wa VETA katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na kuuzwa na Kampuni ya Ujuzi.
Maelezo hayo yametolewa na Ofisa Masoko wa Kampuni Tanzu ya VETA, Ujuzi Incorporated Company Limited, Janeth Nkondora, ambaye ameeleza kuwa kampuni hiyo imekuwa ikitumia ujuzi wa vitendo unaotokana na mafunzo ya VETA kuzalisha bidhaa zenye ubora kwa ajili ya soko.
Kwa upande mwingine, wageni kutoka maeneo mbalimbali wameendelea kutembelea banda la VETA kwa lengo la kupata elimu na taarifa kuhusu mafunzo ya ufundi stadi, fursa zinazopatikana kupitia mafunzo hayo, pamoja na kununua bidhaa mbalimbali zinazouzwa na Kampuni ya Ujuzi.


