Breaking News

UNFPA Yajizatiti Kuboresha Afya ya Mama na Mtoto Tanzania: Lengo Ni Sifuri Vifo vya Uzazi

 


Na Hawa Ismail- Dar es Salaam 

Meneja wa Mawasiliano wa Shirika la United Nations Population Fund (UNFPA), Dkt. Warren Bright, amesema kuwa dhamira kuu ya shirika hilo ni kuhakikisha dunia inakuwa mahali ambapo kila ujauzito unathaminiwa, kila uzazi ni salama, na kila ndoto ya kijana inapata nafasi ya kutimia.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya 12 ya _Tanzania Health Summit_leo Oktoba 2,2025, Dkt. Bright alieleza kuwa UNFPA imejikita katika kutokomeza kabisa vifo vinavyotokana na uzazi, hasa kwa mama na mtoto, kwa kushirikiana kwa karibu na Serikali pamoja na wadau wa sekta ya afya.

“Tunashirikiana vizuri na Serikali pamoja na wadau wa afya ya mama na mtoto kuhakikisha tunafikia sifuri katika lengo hili. Tumekuwa tukiboresha mifumo ya afya ili kufanikisha hilo,” alisema Dkt. Bright.

Katika juhudi za kuboresha huduma za afya, UNFPA imekuwa ikikarabati zahanati, vituo vya afya na hospitali, sambamba na kusambaza vifaa tiba. Dkt. Bright alibainisha kuwa moja ya changamoto kubwa wanazokabiliana nazo ni upotevu wa damu nyingi wakati wa kujifungua. Ili kukabiliana na hilo, shirika hilo limeanzisha benki za damu ambazo husaidia mama kupata damu ya akiba na hivyo kuokoa maisha yake.

Aidha, kwa kina mama wanaojifungua kabla ya muda (watoto njiti), UNFPA imehakikisha kuwa vifaa tiba vinavyosambazwa katika vituo vya afya vina mashine maalum zinazosaidia watoto hao katika makuzi na unyonyeshaji. Dkt. Bright alisisitiza kuwa afya ya mama na mtoto ni kipaumbele cha shirika hilo, na lengo ni kuhakikisha hakuna maisha yanayopotea wakati wa uzazi.

Katika upande wa uzazi wa mpango, Dkt. Bright alieleza kuwa UNFPA inalenga kuhakikisha huduma hizo zinamfikia kila anayezihitaji. Kupitia ushirikiano na Serikali, Bohari ya Dawa (Medical Stores Department), na Wizara ya Afya, shirika hilo linahakikisha huduma za uzazi wa mpango zinapatikana kwa wakati.

Mbali na huduma hizo, UNFPA pia hutoa kondomu, dawa mbalimbali za hospitali, na elimu kuhusu uzazi wa mpango, ikiwemo mabadiliko ya mwili kama uzito wa kupita kiasi. Dkt. Bright alihitimisha kwa kusisitiza kuwa UNFPA itaendelea kujitoa kuhakikisha mama na mtoto wanapata huduma bora na salama.