Dkt.Tindwa aishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kusaidia kupata washiriki zaidi ya 300 kutoka nchi mbalimbali duniani
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanzania Health Summit, Dkt. Chakou Halfani Tindwa, amesisitiza kuwa mafanikio ya sekta ya afya nchini yanatokana na uwepo wa wafanyakazi wenye weledi na ushirikiano thabiti kutoka kwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu
Akizungumza na vyombo vya habari leo, Oktoba 1, 2025, Dkt. Tindwa alieleza kuwa Tanzania Health Summit imekuwa na mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka 12 tangu kuanzishwa kwake. Idadi ya washiriki imeongezeka kutoka 500 hadi zaidi ya 1,500, jambo linaloashiria ukuaji wa ushirikiano na uelewa wa masuala ya afya.
Dkt. Tindwa alieleza kuwa mafanikio ya mara tatu yamepatikana kupitia mchango wa serikali, hususan katika ukusanyaji wa mapato na uendeshaji wa shirika kwa ufanisi. Alisema, “Shirika linaweza kujiendesha lenyewe kwa sasa, jambo ambalo ni mafanikio makubwa chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.”
Katika kipindi kifupi, mipaka imefunguliwa na washiriki kutoka mataifa mbalimbali wameweza kushiriki, wakiwemo mabalozi 11. Hii imeongeza mijadala na mawazo ya kuboresha sekta ya afya na kuchangia juhudi za serikali ya awamu ya sita.
Licha ya kupungua kwa misaada kutoka serikali ya Marekani, Dkt. Tindwa alisisitiza kuwa hakujakuwa na upungufu wa dawa wala huduma duni za afya. “Tumepokea mafanikio makubwa kwa upande wa afya licha ya changamoto hizo,” aliongeza.
Tanzania Health Summit imefanikiwa kuzalisha wataalamu 150 waliopata nafasi ya kuwa viongozi na kutoa elimu juu ya afya bora katika maeneo mbalimbali. Pia, imekuwa jukwaa la kutangaza shughuli za kisayansi na kuieleza dunia mchango wa Tanzania katika sekta ya afya.
