Breaking News

Benki Kuu Yaendelea na Riba ya Asilimia 5.75: Uchumi Waonesha Ustahimilivu na Ukuaji Thabiti

 

Na Hawa Ismail- Dar es Salaam 

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza kuendelea kutumia Riba ya Benki Kuu (CBR) ya asilimia 5.75 kwa robo ya mwisho ya mwaka inayoisha Desemba 2025, hatua inayolenga kuendeleza uthabiti wa uchumi na kudhibiti mfumuko wa bei.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika mkutano na viongozi wa sekta ya benki pamoja na waandishi wa habari, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, amesema kuwa uamuzi huo umetokana na kikao cha Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) kilichofanyika Oktoba 1, 2025. Tathmini ya mwenendo wa uchumi imeonesha kuwa mfumuko wa bei umeendelea kudhibitiwa ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5, huku uchumi ukikua kwa kasi ya kuridhisha.


“Licha ya changamoto za kiuchumi duniani, uchumi wa Tanzania unaendelea kuimarika. BoT itaendelea kusimamia sera ya fedha kwa makini ili kuhakikisha uthabiti wa thamani ya fedha na ukuaji endelevu wa uchumi,” alisema Gavana Tutuba.

Katika robo iliyopita, utekelezaji wa sera ya fedha ulisaidia kuongeza ukwasi katika mabenki, hali iliyochangia kupungua kwa riba za mikopo ya muda mfupi baina ya mabenki hadi kufikia karibu na kiwango cha CBR.

Gavana Tutuba alisisitiza kuwa sera za fedha zimeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kudhibiti mfumuko wa bei na kuchochea shughuli za kiuchumi. Alieleza kuwa katika soko la kimataifa, uchumi wa dunia ulishuhudia kasi ndogo ya ukuaji kutokana na mvutano wa kisiasa na biashara, lakini benki kuu nyingi ziliamua kutopandisha viwango vya riba ili kusaidia uchumi kuimarika. Aidha, bei ya mafuta ghafi duniani ilipungua hadi wastani wa dola 68 kwa pipa, huku bei ya dhahabu ikiendelea kuwa juu, jambo linalotarajiwa kuimarisha mapato ya fedha za kigeni kwa Tanzania.

Kwa upande wa ndani, mfumuko wa bei Tanzania Bara ulikuwa asilimia 3.4 mwezi Agosti 2025, ndani ya lengo la taifa na mashirikisho ya kikanda ya EAC na SADC. Gavana alieleza kuwa uhakika wa chakula, utulivu wa shilingi, na utekelezaji wa sera thabiti za fedha na bajeti umechangia kwa kiasi kikubwa kudhibiti mfumuko huo. Zanzibar nayo ilirekodi mfumuko wa asilimia 4.0, chini ya ukomo wa asilimia 5 unaokubalika.

Katika shughuli za uchumi, Tanzania Bara ilikua kwa asilimia 5.4 katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, huku ukuaji huo ukitarajiwa kuongezeka zaidi katika robo ya pili na ya tatu. Zanzibar ilikua kwa asilimia 6.4, na matarajio ya mwaka mzima kufikia asilimia 7.3, yakichochewa na sekta za utalii, kilimo na ujenzi. Mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka kwa asilimia 15.9, ishara ya kuimarika kwa uhusiano kati ya sekta ya fedha na uchumi halisi.

Gavana Tutuba aliongeza kuwa sekta ya fedha iliendelea kuonesha ustahimilivu, ambapo mikopo chechefu ilipungua hadi asilimia 3.3, chini ya kiwango kinachokubalika cha asilimia 5. Shilingi ya Tanzania ilionyesha uthabiti kwa kuongezeka thamani kwa asilimia 8.4 katika robo ya tatu, huku akiba ya fedha za kigeni ikifikia Dola za Marekani milioni 6.4, kiasi kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kwa zaidi ya miezi mitano.

Akihitimisha taarifa yake, Gavana Tutuba alisema kuwa Kamati ya Sera ya Fedha inatarajiwa kukutana tena Januari 7, 2026, ambapo CBR mpya kwa robo ya kwanza ya mwaka 2026 itatangazwa Januari 8, 2026. Alisisitiza kuwa BoT itaendelea kutekeleza sera zenye kuzingatia uthabiti wa uchumi, maendeleo ya sekta binafsi, na ustawi wa wananchi kwa ujumla.