Tanzania Yaadhimisha Oktoba Kama Mwezi wa Uhamasishaji Dhidi ya Saratani: Wataalamu Wasisitiza Uchunguzi wa Mapema na Ushirikiano wa Kikanda
Tanzania imeungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha mwezi wa Oktoba kama mwezi wa uhamasishaji wa mapambano dhidi ya saratani, hususan saratani ya matiti ambayo inaendelea kuwa chanzo kikuu cha vifo kwa wanawake duniani. Maadhimisho haya yamelenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu ugonjwa huo na kuhimiza uchunguzi wa mapema.
Katika kuadhimisha mwezi huo, kongamano la kimataifa kuhusu saratani limefanyika jijini Dar es Salaam, likiwakutanisha wataalamu wa afya kutoka mataifa mbalimbali. Washiriki walijumuisha madaktari bingwa, watafiti wa afya, na wanaharakati wa afya ya jamii waliobadilishana uzoefu na mikakati ya kukabiliana na saratani.
Rais wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Saratani Tanzania, Dkt. Joel Ndumbaro, alieleza kuwa saratani zote zinaweza kutibika endapo zitagunduliwa katika hatua za awali. “Changamoto kubwa ni kwamba wagonjwa wengi hufika hospitali wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa,” alisema, akisisitiza umuhimu wa uchunguzi wa mapema.
Dkt. Magreth Moshi, Daktari Bingwa wa magonjwa ya saratani, alisisitiza haja ya kuwekeza zaidi katika elimu ya kinga na uchunguzi wa mapema, hasa kwa wanawake na watoto. “Tukianza elimu mapema mashuleni na vijijini, tutajenga kizazi kinachojua namna ya kujikinga,” alieleza.
Dkt. John Thomas kutoka Kenya alieleza kuwa ushirikiano wa kikanda ni muhimu katika kupunguza vifo vinavyotokana na saratani. “Afrika Mashariki inakabiliwa na changamoto zinazofanana. Tukishirikiana katika tafiti na rasilimali, tutaokoa maisha ya maelfu,” alisema.
Mwezi wa Oktoba hutumika duniani kote kuongeza uelewa kuhusu saratani ya matiti. Hata hivyo, wataalamu wanashauri elimu hiyo kupanuliwa pia kwa saratani nyingine zinazoongezeka kwa kasi nchini, ikiwemo saratani ya shingo ya kizazi na tezi dume.



