Doyo Aahidi: Barabara ya Zege Kutoka Dar Hadi Tandahimba, Kusini Kutapewa Kipaumbele
Kilwa, Lindi
Mgombea urais kupitia Chama cha NLD, Mhe. Doyo Hassan Doyo, akiendelea na ziara zake za kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu, amefanya mkutano wa hadhara katika kijiji cha Somanga, wilayani Kilwa, mkoani Lindi.
Katika mkutano huo, Mhe. Doyo amewaahidi wananchi wa Kilwa kuwa endapo watampa ridhaa ya kuongoza nchi, atahakikisha barabara kuu ya kutoka Mbagala, Dar es Salaam hadi Tandahimba inajengwa kwa kiwango cha zege badala ya lami, ili kudumu kwa muda mrefu na kuondoa changamoto zilizopo kwa sasa. alisema Mhe. Doyo, barabara hiyo imechukua muda mrefu kukamilika, na mara nyingi imekuwa ikiharibika kutokana na ubora mdogo wa kazi za baadhi ya wakandarasi,
“Ni wakati sasa tuachane na mtindo wa kujenga barabara za lami zisizodumu. Barabara za zege ndizo suluhisho la kudumu litakalookoa fedha nyingi za wananchi.”
Mhe. Doyo alibainisha kuwa barabara ya ukanda wa kusini imekuwa ikijengwa kwa zaidi ya miaka 40 bila kukamilika, tofauti na barabara zinazounganisha mikoa mingine kama Kaskazini ambazo zimekamilika kwa wakati na kwa ubora wa hali ya juu.
Aidha, Mhe. Doyo aliahidi kuboresha maisha ya wananchi wa Somanga kupitia mikakati ya kuinua uchumi wa vijana na akinamama. Aliahidi kuwapatia vijana zana bora za uvuvi ili kuongeza uzalishaji na kipato, pamoja na kujenga masoko ya kisasa ya uuzaji wa samaki. Pia aliwahakikishia akinamama wajasiriamali kuwa serikali yake itawajengea mabanda bora ya mama lishe, salama na yenye miundombinu rafiki kwa biashara zao.
“Tunataka kila kijana na kila mama awe na mazingira mazuri ya kufanya kazi na kupata kipato. Serikali ya NLD tutakayounda itahakikisha hilo linakwenda kufanyiwa kazi,” alisisitiza Mhe. Doyo.
Msafara wa kampeni wa mgombea huyo uneelekea katika mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, na baadaye Morogoro, kabla ya msafara huo kuelekea mkoa wa Mbeya, Rukwa.
