Breaking News

Tanzania Yaendelea Kung’ara Kimataifa: Watalii Kutoka Urusi Wazidi Kuongezeka

Waziri mwenye dhamana ya Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana amesema kuwa Tanzania imeendelea kuwa _kisiwa cha amani na utulivu_ kutokana na uongozi bora na mahusiano mazuri ya kidiplomasia na mataifa mbalimbali duniani. Hali hiyo imepelekea ongezeko kubwa la watalii kutoka nchi tofauti, hususan Urusi, wanaokuja kujifunza na kufurahia vivutio vya kipekee vya Tanzania.

Akizungumza katika *mkutano wa wahitimu wa vyuo vikuu vya Urusi (Alumni)* uliofanyika jijini Dar es Salaam, Dkt. Chana alibainisha kuwa mkutano huo haukuhusisha Tanzania na Urusi pekee, bali ulihudhuriwa pia na wawakilishi kutoka Kenya, Ghana, Angola na mataifa mengine ya Afrika.

 “Tanzania imekuwa mfano wa amani barani Afrika. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha sekta ya utalii kupitia filamu ya _‘Tanzania: The Royal Tour’_. Kupitia filamu hiyo, miundombinu na maelekezo ya Rais yametekelezwa kwa mafanikio, na sasa watalii kutoka Urusi wameongezeka kwa kasi,” alisema Dkt. Chana.

Kwa mujibu wa Waziri, Tanzania imepokea zaidi ya watalii 12,000 kutoka Urusi* wanaofurahia utalii wa safari, fukwe za Zanzibar, na vivutio vingine vya kipekee. Serikali inaendelea kuimarisha sekta hiyo kwa kuanzisha mazao mapya ya utalii kama vile utalii wa vyakula, utamaduni, na sanaa ili kufikia lengo la *watalii milioni tano* kwa mwaka.

 “Tunaelekea kupokea watalii wasiopungua *bilioni 8* kwa miaka ijayo. Tanzania imekuwa kivutio cha kimataifa, na watu kutoka kote duniani wanatamani kufika hapa,” aliongeza.

Dkt. Chana pia aliwashukuru Watanzania kwa mshikamano wao, akisisitiza kuwa mafanikio ya utalii yanategemea ushirikiano wa wananchi.

 “Watalii wanahitaji huduma mbalimbali kama usafiri wa taxi, migahawa, malazi, na vocha za mawasiliano. Hivyo, kila Mtanzania ananufaika na utalii. Sekta hii inaingiza asilimia *17 ya pato la taifa na asilimia 25 ya fedha za kigeni" alifafanua.

Aidha, Waziri alieleza kuwa *utalii wa mikutano* nao unachangia kwa kiasi kikubwa, huku akitaja ujenzi wa ukumbi mkubwa wa mikutano jijini Arusha, viwanja vya ndege, na barabara za lami kama hatua muhimu zinazochochea ukuaji wa sekta hiyo.

Katika mkutano huo, *mwandishi wa habari kutoka Urusi* alieleza kuwa amejifunza Kiswahili kwa miaka mitano na sasa anajitahidi kuandika habari nyingi kuhusu utalii wa Tanzania. Alisisitiza umuhimu wa kuendeleza elimu, uelewa na ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili.