Breaking News

DCB Yazindua Kampeni ya Kidigitali "The Ground" kwa Ajili ya Wateja wa Kipato cha Chini na Kati

 

Na Hawa Ismail

Dar es Salaam, Oktoba 7, 2025— Benki ya kibiashara ya DCB imezindua kampeni mpya iitwayo _"The Ground"_, inayolenga kuwawezesha wateja kufungua akaunti kidigitali kwa urahisi kwa kutumia simu zao na kitambulisho cha taifa cha NIDA. Kampeni hiyo imezinduliwa rasmi leo jijini Dar es Salaam na inalenga kuleta mapinduzi katika upatikanaji wa huduma za kifedha kwa Watanzania wa kipato cha chini na cha kati.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa DCB na Mkurugenzi wa Mikopo, *Ndugu Deogratius Thadei*, alisema kampeni hiyo itawawezesha wateja kutuma pesa bila makato kupitia simu kwenye mitandao yote, pamoja na kufanya miamala ya benki bila gharama yoyote. Aidha, huduma ya _DCB Lipa Fasta_ itawasaidia wafanyabiashara wadogo kupokea malipo kidigitali kwa haraka na salama.

 “Huduma hii inamwezesha mfanyabiashara kupokea fedha kidigitali na kupokea ujumbe wa kuthibitisha mara moja. Benki ya DCB iliundwa kwa ajili ya watu wa kipato cha chini na cha kati, ambao kila shilingi waliyonayo ni ya thamani. Tunahakikisha hawapotezi hata senti,” alisema Thadei.

Kwa upande wake, *Afisa Masoko wa Huduma kwa Wateja na Huduma za Kidigitali*, _Geofrey Magugu_, alieleza kuwa kampeni hiyo imeletwa mahsusi katika kipindi cha Wiki ya Huduma kwa Wateja ili kuhakikisha kila mteja anapata huduma bila makato.

 “Hii si kampeni ya muda mfupi tu. Tumeamua kuondoa makato kwa kipindi chote cha kampeni na kuendelea kutoa huduma bila makato kwa wateja wetu wote. Lengo letu ni kumuinua mteja na kumrahisishia upatikanaji wa huduma zinazokidhi mahitaji yake,” alisisitiza Magugu.

Katika tukio hilo, *Bi Salma Athumani Mtulia*, mmoja wa wateja wa DCB aliyejiunga na benki hiyo miaka 14 iliyopita, alishiriki kutoa ushuhuda wake. Alieleza kuwa alianza na mkopo wa shilingi laki tano (500,000) na hadi sasa anakopeshwa zaidi ya milioni sita, hali iliyomuwezesha kukuza biashara yake, kununua viwanja, pikipiki na hata kujenga nyumba.

“DCB imenisaidia sana, hata nyakati ngumu walinisikiliza na tukashirikiana kutatua changamoto. Kuondolewa kwa makato ni hatua kubwa kwa wateja kama sisi. Naishukuru DCB kwa huduma zao bora na nawashauri Watanzania kujiunga nao,” alisema Bi Salma.