"KONGAMANO LA AMANI KUFANYIKA DAR ES SALAAM: “MIMI NAAHIDI AMANI SIKU ZOTE”
Katika kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, Taasisi ya Mwanamke na Nguvu ya Kijani (TASSI) imetangaza kongamano la amani litakalofanyika kuanzia Oktoba 25 hadi 27 katika viwanja vya Posta, jijini Dar es Salaam, likiwa na kaulimbiu isemayo _“Mimi naahidi amani siku zote.”_
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa TASSI, Judith Mhina, alisema lengo kuu la kongamano hilo ni kuhimiza uzalendo, mshikamano na kulinda amani ya taifa, hasa katika kipindi cha uchaguzi.
“Wakati tulio nao sasa ni wa Watanzania kusimama pamoja na kulinda amani yetu. Ikivurugika, kila kitu kitaathirika,” alisema Mhina.
Mratibu wa kongamano hilo, Saimon Jacob maarufu kama Rado, alieleza kuwa kongamano hilo litatoa elimu kuhusu historia ya uzalendo wa Tanzania na kuonya dhidi ya maandamano yenye viashiria vya vurugu.
“Tanzania ni nchi yenye amani na uzalendo mkubwa. Wapo wanaotumia siasa kujaribu kuleta machafuko, lakini kupitia kongamano hili tunahamasisha amani,” alisema Rado.
Aidha, alisisitiza kuwa uhuru na amani ni neema kubwa inayopaswa kulindwa na kuthaminiwa na kila Mtanzania.
Kwa upande wake, Rais wa Mitume na Manabii Tanzania, Martin Bashando, aliwataka viongozi wa dini kuwa mstari wa mbele katika kuhubiri amani na mshikamano.
“Amani ni baraka kutoka kwa Mungu. Kila mmoja wetu ana wajibu wa kuilinda, hata vyombo vya habari havipaswi kurusha taarifa zinazoweza kuchochea uvunjifu wa amani,” alisema Bashando.Kongamano hili linatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha viongozi wa dini, wanaharakati, vijana na wananchi kwa ujumla, kwa lengo la kuimarisha misingi ya amani na utulivu wa taifa kuelekea uchaguzi mkuu.
