Breaking News

KAMPENI ZA CCM KIGAMBONI: NYAKISA NA MAFIMBO WAHAKIKISHA MAENDELEO NA AMANI KWA WANANCHI

 


Na Hawa Ismail- Dar es Salaam 

Katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi uliofanyika Oktoba 19, 2025 katika viwanja vya Mradani, Kata ya Tungi, mgombea ubunge wa Jimbo la Kigamboni kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Sanga Haran Nyakisa, aliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kumpigia kura Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na wagombea wa CCM ifikapo Oktoba 29.



Nyakisa alisisitiza umuhimu wa umoja na mshikamano akisema: “Jimbo la Kigamboni lina wapiga kura laki mbili. Naombeni tujitokeze kwa wingi siku hiyo kumpatia kura Rais wetu mpendwa Dkt. Samia, mimi mbunge wenu, na Diwani wa Kata ya Tungi, Ndugu Mafimbo.”

Akielezea mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya CCM, Nyakisa alitaja maendeleo yaliyopatikana katika miundombinu, elimu, afya, ajira kwa vijana, na upatikanaji wa mikopo isiyo na riba.

“Tumeona barabara, hospitali, elimu bure, ajira kwa vijana na mikopo—haya ni matokeo ya utekelezaji wa Ilani ya CCM,” alisema.

Aidha, alitoa wito kwa wananchi wa Kigamboni kudumisha amani na kukataa uchochezi wa mitandaoni:“Ukiona mtu anataka kuvunja amani, ujue hana nia njema na taifa letu. Rais wetu Dkt. Samia ameahidi kuwa Oktoba kutakuwa na amani kama miaka mingine.”

Nyakisa pia aliahidi miradi ya maendeleo kwa Kata ya Tungi, ikiwemo daraja kubwa la kukabiliana na mafuriko, mikopo kwa wanawake na vijana, na ajira mpya kwa walimu na madaktari ifikapo 2026.

Kwa upande wake, mgombea udiwani wa Kata ya Tungi, Ndugu Ernest Mafimbo, aliahidi kushirikiana na viongozi wa juu kuwaletea maendeleo wakazi wa kata hiyo.

“Kata ya Tungi ni mpya, lakini maendeleo yake ni makubwa—ujenzi wa hospitali ya gorofa, barabara za lami, na vituo vya afya vimegharimu bilioni 2.7,” alisema Mafimbo.

Aliongeza kuwa Rais Samia ametenga bilioni 200 kwa ajili ya kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kama mama lishe, baba lishe, bodaboda na machinga, akisisitiza dhamira ya CCM ya kuleta maendeleo kwa makundi yote ya jamii.