Wanahabari Watajwa Kama Nguzo Kuu Katika Mapambano Dhidi ya Saratani – ORCI Yatoa Wito wa Ushirikiano na Elimu kwa Umma
Na Hawa Ismail- Dar es Salaam
Katika kuadhimisha mwezi wa uelewa wa saratani ya matiti (Pink October), Hospitali ya Ocean Road Cancer Institute (ORCI) imeandaa semina maalum kwa wahariri wa vyombo vya habari, ikilenga kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya afya na wanahabari katika mapambano dhidi ya saratani ya matiti.
Dkt. Crispin Kahesa, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, amesisitiza umuhimu wa wanahabari kama daraja la kufikisha elimu sahihi kwa jamii kuhusu ugonjwa wa saratani. “Saratani haibagui. Leo ni huyu, kesho ni mwingine. Wanahabari ni jicho la jamii, na sauti yao ni muhimu katika kuondoa dhana potofu na kuhamasisha uchunguzi wa mapema,” alisema Dkt.Crispin Kahesa
Kwa mujibu wa takwimu alizotoa, takribani wanawake 4,500 huathiriwa na saratani ya matiti kila mwaka nchini Tanzania, huku mmoja kati ya wawili akipoteza maisha ndani ya kipindi cha miaka mitano. Aidha, ni wanawake watano tu kati ya kila 100 wanaojitokeza kwa uchunguzi wa awali.
Dkt. Johnson Katanga aliongeza kuwa mwaka 2022, dunia ilishuhudia wagonjwa wapya wa saratani wapatao milioni 22, huku milioni 9.7 wakipoteza maisha. Tanzania ilirekodi wagonjwa wapya 29,000, ambapo 743 walifariki kutokana na saratani ya matiti pekee. Saratani ya matiti inachangia asilimia 60 ya saratani zote nchini.
Dkt. Katanga alieleza kuwa viatarishi vya saratani vinavyoweza kuepukika ni pamoja na uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe kupita kiasi, kutofanya mazoezi, na ulaji usiofaa. Viatarishi visivyobadilika ni pamoja na umri, historia ya familia, na jinsia. Alisisitiza umuhimu wa elimu ya kinga, mazoezi, na chanjo kama HPV na HB kwa watoto na watu wazima.
ORCI inatoa huduma mbalimbali ikiwemo uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi, matiti, saratani ya ngozi, na saratani ya tezi dume. Dkt. Kahesa alieleza kuwa hospitali hiyo inatarajia kusherehekea miaka 30 ya utoaji huduma mwaka 2026, huku ikilenga upatikanaji wa huduma kwa usawa bila kujali uwezo wa kifedha wa mgonjwa.
Dkt. Maguhwa Stephano alieleza kuwa saratani ya matiti ni ya pili kwa ukubwa duniani na kitaifa, lakini inaweza kuzuilika iwapo itagunduliwa mapema. Alisisitiza umuhimu wa lishe bora, unyonyeshaji, na uchunguzi wa mara kwa mara. Tiba zinazopatikana nchini ni pamoja na mionzi, kemia, na upasuaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Bi. Batuli Ramadhani na Ostadhi Ramadhani Musha walitoa ushuhuda wa safari yao ya matibabu, wakieleza changamoto na mafanikio waliyopata kupitia huduma za ORCI. Waliomba serikali kuimarisha upatikanaji wa dawa na huduma kwa wagonjwa wote bila ubaguzi.
Fredrick Ludovick alihitimisha kwa kusema kuwa matibabu ya mionzi ni salama na yenye ufanisi mkubwa. Alisisitiza kuwa si kila uvimbe unahitaji upasuaji, na kwamba tiba hutegemea aina ya saratani na hatua iliyofikia. “Saratani inatibika. Tujipende, tujichunguze, na tuanze matibabu mapema,” alihimiza.








