Doyo: NLD Itaondoa Mfumo wa Stakabadhi Ghalani Kuwasaidia Wakulima wa Korosho.
TANDAHIMBA, MTWARA
Mgombea Urais kupitia Chama cha NLD, Mhe. Doyo Hassan Doyo, ameendelea na kampeni zake za kuomba ridhaa ya wananchi katika Wilaya ya Tandahimba, mkoani Mtwara, ambako alipokelewa na wafuasi wa chama hicho pamoja na wakazi wa maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Katika hotuba yake kwa wananchi wa Tandahimba, Mhe. Doyo aligusia changamoto kadhaa zinazowakabili wakazi wa wilaya hiyo, hususan wakulima wa zao la korosho, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamikia mfumo wa stakabadhi ghalani unaodaiwa kupunguza tija kwa mkulima wa chini.
“Mfumo huu wa stakabadhi ghalani umegeuka kuwa kikwazo kwa wakulima. Wakulima wanachoka kulima, kwasababu wanavuna umasikini. Serikali ya NLD itahakikisha tunauondoa mfumo huu na kuweka utaratibu wa soko huria utakao mlipa mkulima kwa haki na kwa wakati,” alisema Mhe. Doyo huku akishangiliwa na umati wa wananchi.
Aidha, Mhe. Doyo aliahidi kufanya maboresho makubwa katika miundombinu ya barabara, hususan barabara za vijijini ambazo zimekuwa zikisababisha ugumu wa usafirishaji wa mazao ya wakulima kutoka mashambani hadi sokoni.
“Tandahimba haiwezi kuendelea ikiwa barabara zake hazipitiki wakati wa mvua. Tutahakikisha barabara za vijijini zinajengwa kwa kiwango kinachorahisisha biashara na usafiri wa wananchi wote,” alisisitiza.
Katika sekta ya afya, Mhe. Doyo alizungumzia upungufu wa vituo vya afya na dawa katika hospitali za wilaya na vijiji, akiahidi kuongeza bajeti ya afya na kusimamia utoaji wa huduma kwa uwiano wa kitaifa.
“Mama mjamzito wa Tandahimba anapaswa kupata huduma sawa na mama wa Dodoma au Dar es Salaam. NLD itaimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na watumishi wa afya katika kila kijiji,” alisema Mhe. Doyo.
Doyo aliwataka wananchi wa Tandahimba kufanya maamuzi sahihi katika uchaguzi ujao kwa kuchagua chama kinachoangalia maslahi ya mkulima, mfanyabiashara na kijana wa kawaida.
“Tunataka Tanzania yenye usawa wa kiuchumi, ambapo Tandahimba itasikika kama Dodoma. NLD ni sauti ya mabadiliko hayo,” alihitimisha.
Kwa upande wake, mgombea ubunge kupitia chama hicho, Ndugu Said Mussa Mombita, alizungumzia changamoto zinazowakabili wananchi wa Tandahimba, ikiwemo upatikanaji wa maji, zao la korosho, na huduma za afya.
Mombita alisema kuwa endapo wananchi watamchagua kuwa mbunge wao, ataweka kipaumbele katika kusikiliza ushauri wa wananchi na kuyawasilisha maoni hayo kama ajenda kuu za utekelezaji wake.
“Ni lazima wananchi wa Tandahimba tuwe na vipaumbele vyetu muhimu ili tuweze kuweka mikakati madhubuti ya kupigania maendeleo yetu. Nichagueni ili niwe chombo cha kuwatumikia ipasavyo,” alisema Mombita.
Msafara wa kampeni wa mgombea urais huyo wa NLD unaelekea Lindi, hususan Wilaya ya Masasi, Lindi Mjini na Somanga, kuendelea na mikutano ya hadhara.


