WASIFU NA HISTORY YA MHE. DOYO HASSAN DOYO, MGOMBEA URAIS WA JAMHUR YA MUUNGANO WA TANZANIA
Utangulizi
Mhe. Doyo Hassan Doyo ni mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kupitia Chama cha National League for Democracy (NLD). Safari yake ya maisha na siasa imekuwa na changamoto nyingi, ikimjenga kuwa mwanasiasa mwenye msimamo thabiti na dira ya mabadiliko.
Maisha ya Awali
Doyo alizaliwa alfajiri ya Januari 1, 1974 katika Kijiji cha Misima, Kata ya Misima, Wilaya ya Handeni, Mkoa wa Tanga. Yeye ni mtoto wa Mohammed Doyo na Zaina Jira. Alipozaliwa, alipewa jina la Hassan Mohammed Doyo.
Mwaka 1983, akiwa na umri wa miaka tisa, aliandikishwa katika Shule ya Msingi Misima, Handeni. Hapo ndipo safari yake ya elimu ilipoanza. Miaka kadhaa baadaye, akiwa likizo, alishuhudia tukio lililobadili maisha yake. mama yake, Zaina, alikamatwa na maofisa wa kodi kwa kushindwa kulipa kodi ya kichwa ya shilingi 200. Hili lilimwachia doa la kudumu akilini na kumfanya kuapa kuwa mwanasiasa, akiamini kuwa uongozi wa haki hauna budi kuondoa unyanyasaji dhidi ya wananchi wanyonge.
Safari ya Elimu
Baada ya kuhitimu elimu ya msingi mwaka 1989, Doyo alihamia Dar es Salaam na kujiunga na Shule ya Seminari ya Kiislam ya Masjid Quba, ambapo alisoma hadi mwaka 1993. Mwaka 1998, alianza masomo katika Chuo cha Dar City, akisomea Mawasiliano ya Umma, Utangazaji na Uhusiano wa Umma hadi mwaka 2001 (ngazi ya cheti na diploma).
Elimu yake ya juu pia ilijumuisha.
Kozi ya Mikakati ya Uchaguzi, Hamburg, Ujerumani (2003).
Kozi Chuo cha Taifa cha Ulinzi cha Jeshi, (National Defence College, NDC) kilichopo Kunduchi, Dar es Salaam. Kozi namba (Capstone 17, 2024)
Masomo ya Ujengaji wa Migodi na Utambuzi wa Miamba, Chuo cha Madini Dodoma (2011).
Safari ya Kisiasa
Doyo aliingia rasmi katika siasa Februari 25, 1993, akiwa na miaka 19, alipojiunga na Chama cha Wananchi (CUF). Uanachama wake ulithibitishwa na Mwenyekiti wa kwanza wa chama hicho, James Mapalala.
Ndani ya CUF, alipanda ngazi kutoka mwanachama wa kawaida hadi kuwa Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Handeni (1996/2011). Alidumu katika nafasi hiyo kwa miaka 15 na pia alikuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa la Uongozi wa CUF.
Mnamo Januari 4, 2011, alifukuzwa uanachama kutokana na tofauti za msimamo na viongozi wa juu wa chama. Baada ya hapo, alihamia na kuasisi chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) kilichosajiliwa rasmi Agosti 22, 2012.
Katika ADC, alishikilia nafasi mbalimbali zikiwemo.
Mlezi wa Kanda ya Kaskazini (2012).
Mkurugenzi wa Habari (2013/2014).
Naibu Katibu Mkuu Bara (2014/2016).
Katibu Mkuu wa Taifa (2016/2024).
Mwaka 2024, aligombea Uenyekiti wa Taifa wa ADC lakini hakufanikiwa. Baadaye alihamia NLD, akachaguliwa kuwa Katibu Mkuu na hatimaye mgombea urais wa chama hicho mwaka 2025.
Ajenda na Itikadi
Katika kampeni zake, Doyo ameweka mbele ajenda kuu sita.
1. Ajira
2. Afya
3. Elimu
4. Miundombinu
5. Kilimo
6. Mapambano dhidi ya rushwa
Anasisitiza juu ya matumizi bora ya rasilimali za taifa ili kutoa ajira, kuimarisha sekta ya kilimo, kuboresha elimu yenye tija na kukomesha kabisa ufisadi. Pia ameahidi kuanzisha Kituo cha Utafiti wa Kisayansi na kufuta mfumo wa elimu wa sasa unaodaiwa kukosa manufaa kwa wahitimu.
Maisha Nje ya Siasa
Kati ya 1996 na 2000, Doyo anakiri kupitia kipindi kigumu bila kipato cha uhakika, hali iliyomsababisha kumrudisha mkewe wa kwanza nyumbani kwa wazazi wake ili ajipange upya. Hata hivyo, amejijengea jina nje ya siasa kama mchimbaji mkubwa wa madini ya viwandani, akimiliki zaidi ya migodi 50 na kuajiri mamia ya vijana. Pia ni mkulima wa katani na mazao ya chakula.
Familia
Doyo ni mume wa wake wawili.
Lina Burhani Kilo (anaishi Tanga)
Halima Rajab Msumari (anaishi Dar es Salaam)
Wana watoto watano.
1. Fahdi, mwanafunzi wa IFM, anayesomea Shahada ya Usalama wa Mtandao na mgombea ubunge Kawe 2025.
2. Ibad, mhitimu wa stashahada ya Maendeleo Vijijini, sasa yupo JKT.
3. Zakati, mwanafunzi wa biashara, Kibaha.
4. Awena, darasa la tano.
5. Ummy, darasa la pili.
Baba yake, Mohammed Doyo, naye aliwahi kushiriki kwenye siasa akiwa mjumbe wa serikali ya mtaa na mjumbe wa CCM katika kijiji chao cha Misima.
Safari ya maisha ya Mhe. Doyo Hassan Doyo imejengwa na changamoto ya maisha, elimu, na uzoefu wa siasa unaoenea zaidi ya miongo mitatu. Kuanzia simulizi la mama yake kukamatwa kwa kodi ya kichwa hadi leo akiwa mgombea urais kupitia Chama cha NLD, Doyo anaamini kwamba Tanzania yenye Uzalendo,haki na maendeleo inapatikana kupitia uongozi unaoweka mbele maslahi ya wananchi wote.
Huyu ndiye Doyo Hassan Doyo, mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mzigua kutoka Misima, Handeni, Tanga. Ni mgombea hodari anayefanya kampeni zake kwa mtindo wa Mobile kampeni, huku akijenga hoja zinazowavutia Watanzania wengi, ni mgombea pekee anayewafuata wapiga kura mahali walipo ili kuwapelekea sera zinazotokana na Ilani Bora ya Chama cha NLD, Ilani inayongozwa na dira ya Uzalendo, Haki, na Maendeleo.
