*NIDA Yasherehekea Siku ya Vitambulisho Duniani kwa Kuwatambua Walemavu Temeke
Katika maadhimisho ya kilele cha Siku ya Vitambulisho Duniani yaliyofanyika tarehe 17 Septemba 2025 katika Manispaa ya Wilaya ya Temeke, Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji wa Vitambulisho, Ndugu Edson Guyai, amesema kuwa lengo kuu la Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata utambulisho rasmi ifikapo mwaka 2030.
Maadhimisho hayo yaliandaliwa kwa ushirikiano na Idara ya Ustawi wa Jamii Temeke, yakilenga kutoa elimu na huduma kwa kundi la watu wenye ulemavu. Kauli mbiu ya mwaka huu ilikuwa _"Utambulisho Wangu, Mwamvuli Wangu"_, ikisisitiza umuhimu wa kitambulisho cha taifa kama kinga na nyenzo ya ushiriki kamili katika jamii.
Guyai alieleza kuwa walichagua kundi la walemavu kutokana na changamoto wanazokumbana nazo, ikiwemo ulemavu wa kuona na wa viungo, hali inayowafanya kuwa na ugumu wa kupata huduma kwa urahisi. Alisisitiza kuwa NIDA inalenga kutoa huduma kwa makundi yote ya jamii, lakini walemavu wanahitaji msaada wa ziada ili waweze kusajiliwa na kutambulika rasmi katika nyanja za kisiasa, kidini na kiuchumi.
“Lengo la NIDA ni kutoa huduma kwa makundi yote. Lakini kutokana na changamoto wanazokumbana nazo walemavu, tumeona ni muhimu kuwasajili, kuwatambua na kuwapatia vitambulisho vinavyowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kijamii,” alisema Guyai.
Aidha, alisisitiza kuwa kauli mbiu ya NIDA ni _"Jisajili, Kutambue na Tukutambulishe"_, ikiwa ni mwongozo wa kuhakikisha kila kundi linapata huduma stahiki. Aliongeza kuwa maoni kutoka kwa walemavu wa Temeke yatatumika kuboresha huduma kwa nchi nzima.
Afisa Ustawi wa Jamii na Mratibu wa Watu Wenye Ulemavu Wilaya ya Temeke, Bi. Restituta Simon Bujiku, aliipongeza NIDA kwa hatua hiyo, akisema kuwa ni mfano wa kuigwa kwa kuwashika mkono makundi yenye uhitaji.
“Tunashukuru kwa kutambua mahitaji ya walemavu na kuchagua wilaya yetu kuwa mfano. Ni jambo la kujifunza na linaonesha dhamira ya kweli ya kuwajumuisha wote,” alisema Bujiku.
Kwa upande wake, Bw. Juma Mlawa, mmoja wa walemavu waliohudhuria, alieleza furaha yake kwa kutambuliwa na kusajiliwa rasmi na NIDA. Alisema zoezi hilo limewasaidia kupata vitambulisho pamoja na zawadi ya miamvuli, na limewafundisha umuhimu wa kitambulisho cha taifa katika maisha ya kijamii.
“Tumejifunza kuwa kitambulisho cha taifa ni nyenzo muhimu inayotuwezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kisiasa, kiuchumi na kijamii,” alisema Mlawa.







