Breaking News

Japani na Tanzania Zaunganisha Nguvu Kukuza Biashara ya Kaboni na Teknolojia Safi

 


Na Hawa Ismail – Dar es Salaam_

Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Japani imezindua rasmi Kamati ya Pamoja ya Biashara ya Kaboni, hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Uzinduzi huo umefanyika leo jijini Dar es Salaam, ukihudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka sekta za mazingira na maendeleo endelevu. Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Cyprian Luhemeja, amesema kamati hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Japani katika utekelezaji wa miradi ya kaboni yenye tija kwa taifa.

Mhandisi Luhemeja amefafanua kuwa kamati hiyo itarahisisha uratibu wa kitaalamu na kutoa ushauri wa kisera, sambamba na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje katika sekta za nishati safi, kilimo endelevu, na uhifadhi wa mazingira.

Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Japani nchini Tanzania, Mhe. Ueda Shoichi, amesema kuwa ushirikiano huo ni ishara ya dhamira ya Japani kushirikiana na Tanzania katika biashara ya kaboni, teknolojia, uwekezaji na maendeleo endelevu. Ameongeza kuwa hatua hiyo itaongeza nguvu katika kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kijamii kati ya mataifa hayo mawili.