TANZANIA YAPOKEA EURO MILIONI 370 KWA MAENDELEO YA UCHUMI WA BULUU
![]() |
| Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Abdalah Mitawi, akifungua Kongamano la Kitaifa la Wadau wa Uchumi wa Buluu 2025 |
Na: Kelvin Kijo
Wadau wa sekta ya bahari nchini Tanzania wamekutana katika Kongamano la Kitaifa la Uchumi wa Buluu 2025 kwa lengo la kujadili fursa, changamoto, na mikakati ya kuendeleza uchumi unaotokana na rasilimali za maji.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, leo tarehe 10 Septemba 2025 jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Abdalah Mitawi, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya wadau wa sekta ya bahari katika kusukuma mbele maendeleo ya uchumi wa buluu.
“Tunashukuru Umoja wa Maendeleo ya Ulaya kwa mchango wa shilingi Euro milioni 370, ambao utasaidia kuimarisha sekta hii muhimu,” alisema Mhe. Mitawi.
Katika hotuba yake, Mhe. Mitawi alitaja baadhi ya rasilimali zinazoweza kuchochea uchumi wa buluu nchini,
“Samaki aina 33 wa maji chumvi na 17 wa maji baridi, gesi asilia Futi za ujazo trilioni 47.13 baharini, bandari 86 rasmi na 885 zisizo rasmi, maji baridi Km² 61,500 yenye uwezo wa kutoa m³ bilioni 126 kwa mwaka, umwagiliaji Hekta milioni 29.4 zinazofaa kwa kilimo, misitu ya Pwani Km² 700, mikoko Km² 1,440 (kulingana na mkakati wa 2025–2035), miamba ya Matumbawe Km² 3,580, maeneo ya hifadhi Km² 307,800 (32.5% ya eneo la nchi)” amesema Mhe. Mitawi.
Katika kuonyesha mshikamano wa kimataifa, Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya (EU), Daniel Gonzalez, alieleza dhamira ya EU katika kusaidia Tanzania kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Uchumi wa Buluu ya mwaka 2050.
“Tunaona tija katika kutunza mazingira yanayotuzunguka, kuendeleza utalii, na kutumia rasilimali za majini kwa uendelevu. Tunasimama pamoja na Tanzania kuimarisha maono ya uchumi wa buluu, na kwa hilo tumetenga fedha na kuanzisha miradi kwa kushirikiana na nchi za Sweden, Ujerumani na Umoja wa Ulaya,” alisema Gonzalez.
![]() |
| Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya (EU), Daniel Gonzalez |
Mkurugenzi wa Miundombinu kutoka Wizara ya Uchukuzi, Mhandisi Shomari Shomari, alieleza kuwa serikali imefanya maboresho makubwa ya bandari nchini, hatua iliyochangia kuimarisha usafirishaji wa majini na utekelezaji wa sheria.
“Licha ya mafanikio haya, bado tunakabiliwa na changamoto ya malori bandarini. Tunawahimiza wasafirishaji kuchangamkia fursa za uchumi wa buluu,” alisema Mhandisi Shomari.
![]() |
| Mkurugenzi wa Miundombinu Wizara ya Uchukuzi Mhandisi Shomari Shomari |
Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Profesa Tumaini Gurumo, alieleza kuwa kongamano hilo limejumuisha wadau kutoka wizara mbalimbali, ikiwemo kilimo, uvuvi, na uchukuzi.
“Tunalenga kufanya tathmini ya maendeleo ya uchumi wa buluu tangu 2021 hadi sasa, na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto zilizopo,” alisema Profesa Gurumo.
![]() |
| Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Profesa Tumaini Gurumo |
Aliongeza kuwa kongamano hilo ni sehemu ya Dira ya Maendeleo ya Uchumi wa Buluu ya mwaka 2050, inayolenga kuimarisha sekta hiyo kwa kiwango cha kimataifa.
Kongamano hili linalofanyika kwa siku mbili Septemba 10 na 11 limewezeshwa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Uchukuzi kupitia DMI, Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi ya Zanzibar.







