Breaking News

SPEK Yajivunia Teknolojia ya Kisasa Katika Utengenezaji wa Mabomba

Na Hawa Ismail- Dar es Salaam 

Dar es Salaam— Kampuni ya SPEK inayojishughulisha na utengenezaji wa mabomba kwa matumizi ya gesi, kilimo, ujenzi, migodi na usafirishaji wa maji, imesema kuwa mafanikio yake katika kudumisha mahusiano ya kuaminika na wateja yanatokana na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika uzalishaji wa bidhaa zake.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Afisa Masoko wa kampuni hiyo, Bi. Hafifa Bahfif, alieleza kuwa kuimarika kwa kampuni hiyo ya Kitanzania kumeleta fahari kwa wateja wa ndani na nje ya nchi, kutokana na ubora wa huduma na bidhaa wanazozalisha.

“Sisi kama SPEK tunajivunia teknolojia ya kisasa. Mashine zetu zina uwezo mkubwa na ni za kisasa zaidi ukilinganisha na viwanda vingine vinavyohusika na utengenezaji wa mabomba. Hii ndiyo sababu kubwa inayotujengea uaminifu kwa wateja wetu,” alisema Bi. Hafifa.

Aidha, alibainisha kuwa kampuni hiyo imefanikiwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima nchini, hususan katika sekta ya umwagiliaji.

“Hatujawasahau wakulima. Tumezalisha mabomba ya aina mbalimbali yanayosaidia kusambaza maji mashambani, jambo ambalo litachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uzalishaji wa mazao. Maendeleo ya kilimo hayawezekani bila maji,” aliongeza.

Bi. Hafifa pia alieleza kuwa SPEK ina hamasa kubwa ya kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) pamoja na viwanda vinavyotumia nishati ya gesi katika mikoa mbalimbali nchini na hata katika mataifa ya nje.