Breaking News

DAR ES SALAAM GLASS WORKS YATANGAZA UBORA NA USALAMA WA KIMATAIFA


Na mwandishi wetu

Kampuni kongwe ya utengenezaji vioo, Dar es Salaam Glass Works, imeibuka upya kwa msisitizo kuwa bidhaa zake ni salama na zenye ubora wa viwango vya kitaifa na kimataifa.

Akizungumza katika maonyesho ya Wahandisi yaliyofanyika Upanga jijini Dar es Salaam, Afisa Masoko wa kampuni hiyo, Hassanaly Dastoor Talib, alisema usalama ndio nguzo kuu ya kila mradi wao.

“Tunaposhughulika na vioo, tunalinda maisha ya Watanzania, wafanyakazi wetu na uimara wa jengo. Wateja wetu waamini kuwa tunasimama kidete kuhakikisha usalama kwanza,” alisema Talib kwa msisitizo.

Kwa zaidi ya miaka 45 ya uzoefu, kampuni hiyo imekuwa kinara katika sekta ya vioo nchini tangu ilipoanzishwa mwaka 1979. Talib alifichua kuwa wao ndio wa kwanza kuingiza teknolojia ya kisasa ya vioo nchini kupitia sekta binafsi, jambo lililowaweka mstari wa mbele katika ubunifu na uimara.

Kampuni hiyo inajivunia kuzalisha vioo vya daraja la juu, vya aina mbalimbali vinavyokidhi mahitaji ya kila mradi – kutoka majengo makubwa ya serikali hadi miradi ya binafsi.

Miradi iliyothibitisha ubora wao inajumuisha: jengo la Airtel, Majengo ya wizara mbalimbali Dodoma, Majengo ya biashara ya kisasa jijini Dar es Salaam na kwingineko.

Kwa mujibu wa Talib, dhamira ya kampuni ni kuendelea kuwa nguzo ya ujenzi salama na wa kisasa Tanzania.