Mkutano wa Wanawake Afrika Katika Sekta ya Afya na Usalama Kazini Wafanyika Tanzania, Wadau Wataka Usawa na Maendeleo Jumuishi
Na Mwandishi Wetu-Dar es Salaam
Rais na mmiliki wa taasisi ya SOWSHEA, Bi Funmi Adegbola, amesema kuwa mikutano kama huu ni jukwaa muhimu linalowaunganisha wanawake waliotangulia katika taaluma ya Afya, Usalama na Makazi na wale wanaoendelea kujifunza. Akizungumza katika Mkutano wa Wanawake Afrika wanaofanya kazi katika sekta ya Afya, Usalama na Mazingira Kazini (Africa Women in EHS), Bi Adegbola alisisitiza umuhimu wa ushirikiano na mafunzo endelevu kwa maendeleo ya sekta hiyo.
Mkutano huo mkubwa wa kimataifa ulifanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 26 hadi 27 Septemba 2025, na uliwakutanisha washiriki 200 kutoka nchi saba barani Afrika. Bi Adegbola alieleza kuwa mada kuu zilijikita katika namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, matumizi ya akili mnemba na teknolojia kwa ajili ya kujiandaa na kuleta maendeleo endelevu.
![]() |
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa Ukanda wa Afrika Mashariki, Bi Caroline Khamati Mugalla, alisema kongamano hilo limewaleta pamoja wanawake wanaofanya kazi katika mazingira yanayohitaji usafi na usalama. Alisisitiza kuwa lengo kuu ni kujadili mchango wa wanawake katika kuboresha mazingira ya kazi, hasa kwa kutumia akili mnemba na teknolojia.
“Usalama wa mahali pa kazi haupaswi kuzingatia jinsia, ulemavu au umri. Tunapaswa kuhakikisha kila mtu anafanya kazi katika mazingira salama na yenye afya,” alisisitiza Bi Mugalla.
Naye Mwenyekiti wa TOHASA, Bi Gloria Ivera, alieleza kuwa taasisi hiyo inaleta pamoja wataalamu wa Afya, Usalama na Mazingira kwa lengo la kutoa mafunzo ya bure na kuhamasisha ushirikiano kazini. Alisema kuwa hata wale wasio na uzoefu wanaweza kujifunza kupitia taasisi hiyo.
“Tunatoa fursa kwa kila mmoja, kuanzia mama ntilie hadi wachimbaji madini, kwa kuhakikisha usalama wa makazi na mazingira ya kazi. Tunapozungumzia maendeleo ya kisasa, ni lazima tusimuache mtu nyuma,” alisema Bi Ivera.
Mkutano huo umeweka msingi wa majadiliano ya kisera na kimkakati kuhusu usalama wa mahali pa kazi, huku wadau wakisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kitaifa na kikanda katika kuhakikisha mazingira salama kwa wote.




