Waziri Ulega Atoa Onyo kwa Wahandisi Wanaokiuka Maadili, Aitaka ERB Kuchukua Hatua
Na Hawa Ismail- Dar es Salaam
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, ameitaka Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kuchukua hatua kali za kinidhamu dhidi ya wahandisi wanaokiuka maadili ya kazi, wasiozingatia viapo vya taaluma na wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa kufunga maadhimisho ya 22 ya Siku ya Wahandisi Tanzania, yaliyobeba kauli mbiu _“Wajibu wa Wahandisi kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050”_, Waziri Ulega alisisitiza umuhimu wa wahandisi kutekeleza miradi kwa weledi ili kulinda heshima ya taaluma, usalama wa wananchi na rasilimali za taifa.
Aidha, Waziri Ulega aliipongeza ERB kwa kuanzisha utaratibu wa kutoa zawadi kwa wanafunzi wanaoonyesha juhudi na vipaji katika taaluma ya uhandisi, akisema hatua hiyo inaleta hamasa na kuendeleza kizazi cha wahandisi mahiri. Alitoa wito kwa ERB kushirikiana na wadau mbalimbali ili kudhamini tuzo hizo na kupanua wigo wa ushiriki.
Katika hatua nyingine, Waziri aliagiza ERB kuwasilisha mapendekezo yote yaliyotokana na mkutano huo kwa Wizara ya Ujenzi ili yafanyiwe kazi kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kiuchumi nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wakandarasi, Mhandisi na Mwanasheria Mhe. Mwenye Manga, alieleza kuwa mkutano huo umehudhuriwa na wakandarasi takriban 4,500 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania. Alifafanua kuwa mada kuu zilizojadiliwa zilihusu mchango wa wakandarasi katika kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.
“Zilikuwa mada saba zilizowasilishwa na wahandisi, zikiangazia maeneo muhimu ya ushiriki wao katika kufanikisha dira ya 2050,” alisema Mhe. Manga.
Maadhimisho ya mwaka huu yamevutia zaidi ya wahandisi 4,000 kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwemo washiriki kutoka India, Ethiopia, Uganda na Kenya. Wahandisi wapatao 400 walikula kiapo cha utiifu, ishara ya kujitolea kwao kuhudumia taifa kwa uadilifu na uaminifu.


