Breaking News

UHITAJI WA MAFUTA WACHOCHEA UPANUZI MKUBWA WA BIASHARA YA UAGIZAJI NCHINI



Na Kelvin Kijo - Dar es Salaam 


Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja nchini (PBPA) umetangaza mafanikio makubwa katika sekta ya mafuta, huku kampuni za uagizaji zikiwa zimeongezeka maradufu katika kipindi cha miaka minne – kutoka kampuni 33 mwaka 2021 hadi 73 kufikia mwaka 2025. Sambamba na hilo, jumla ya wazabuni 24 wameweza kusajiliwa rasmi kwa ajili ya kushiriki katika zoezi la kuagiza mafuta kwa pamoja.


Akizungumza na waandishi wa habari leo, tarehe 7 Agosti 2025 jijini Dar es Salaam, katika mkutano ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mkurugenzi Mkuu wa PBPA, Bw. Erasto Mulokozi, alisema ongezeko hilo ni matokeo ya uhitaji mkubwa wa mafuta nchini, hali iliyochochea ongezeko la kiwango cha mafuta yanayoagizwa kutoka tani 5,805,193 mwaka 2021 hadi kufikia tani 6,365,986 mwaka 2025 – ikiwa ni ongezeko la asilimia 9.6.

Aidha, PBPA inatarajia kiwango hicho kufikia tani 7,090,165 kufikia Desemba 2025, ikiwa ni ongezeko zaidi la asilimia 11.4. “Tunaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mikataba ya zabuni, ratiba za meli na huduma za bandari ili kuhakikisha shehena zote zinaingia kwa wakati na kukidhi mahitaji ya ndani,” alisema Bw. Mulokozi.


Katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa mafuta au ucheleweshwaji wa uingizaji, serikali imechukua hatua madhubuti kwa kushirikiana na PBPA kuongeza idadi ya maghala ya kuhifadhia mafuta. Kutoka maghala 22 mwaka 2021, sasa yamefikia 24 mwaka 2025, huku uwezo wa kuhifadhi ukiongezeka kutoka lita milioni 1,288.101 hadi kufikia lita milioni 1,721.327.


Bw. Mulokozi alibainisha kuwa mafanikio haya yanachangiwa pia na ushirikiano mzuri kati ya taasisi mbalimbali za serikali kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Viwango (TBS), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Wakala wa Vipimo (WMA), na EWURA.


Katika kipindi cha utawala wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, PBPA imepokea wageni mbalimbali kutoka nchi jirani zikiwemo Zambia, Mozambique, Burundi, Rwanda, Uganda, Zimbabwe na Namibia waliokuja kujifunza kuhusu mfumo wa Tanzania wa kuagiza mafuta kwa pamoja. Hii ni ishara kuwa Tanzania imeendelea kuwa mfano wa kuigwa katika usimamizi bora wa nishati ya mafuta.


Kwa ujumla, hatua hizi zinaonesha dhamira ya serikali kuimarisha usalama wa nishati nchini huku ikiweka mazingira mazuri ya biashara na ushirikiano wa kikanda kwa maendeleo ya kiuchumi ya Tanzania na majirani zake.