Mpina Atangazwa Mgombea Urais wa ACT Wazalendo 2025
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Chama cha ACT Wazalendo kimemchagua rasmi Luhaga Joelson Mpina kuwa mgombea wake wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Uamuzi huo umetangazwa katika Mkutano Mkuu Maalum wa chama uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Katika mchakato wa upigaji kura ulioshirikisha wajumbe 610, kura halali zilizohesabiwa zilikuwa 605 huku kura tano zikiwa zimeharibika. Ndg. Mpina alipata ushindi wa kishindo kwa kura 559 dhidi ya mpinzani wake, Ndg. Aaron Kalikawe, aliyepata kura 46 pekee.
Pamoja na hilo, ACT Wazalendo imemteua Bi. Fatma Abdulhabib Ferej kuwa mgombea mwenza wa urais. Wawili hao sasa wanaunda timu ya kugombea nafasi ya juu kabisa ya uongozi wa nchi kupitia tiketi ya chama hicho.
Uteuzi huu unafungua rasmi ukurasa wa kampeni za uchaguzi kwa upande wa ACT Wazalendo, ambao wamesisitiza dhamira yao ya kuleta mabadiliko ya kweli ya kisiasa na kiutawala nchini Tanzania.


